📌 Dkt. Biteko asema suala la kuwapa nishati wananchi sio hiari
📌 Asisitiza miradi ya usafirishaji umeme EAPP kukamilika kwa wakati
📌 Vyanzo vipya vya umeme kuendelezwa kukidhi mahitaji
Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Mawaziri wanaohusika na mfumo wa pamoja wa umeme kwa nchi za Mashariki mwa Afrika (EAPP Council of Ministers-COM) limekubaliana kwa pamoja kuwa na usimamizi madhubuti wa miradi mbalimbali ya umeme katika nchi wanachama, ili iweze kukamilika kwa wakati na kuwapatia wananchi nishati ya kutosha.
Kukamilika kwa miradi kutoka vyanzo mbalimbali vya umeme, kutawezesha nchi hizo kusaidiana pale nchi mojawapo inapokuwa na upungufu wa umeme huku msisitizo ukiwekwa kwenye miradi ya usafirishaji umeme.(Transmission lines).
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko tarehe 27 Februari 2024 katika Mkutano wa 18 wa Baraza la Mawaziri wanaohusika na mfumo wa pamoja wa umeme kwa nchi za Mashariki mwa Afrika (EAPP Council of Ministers-COM) ambao unafanyika kwa siku mbili jijini Nairobi, Kenya.
“ Baraza hili ni muhimu katika kuhakikisha nchi za Afrika zinaungana kwa ajili ya kuendeleza rasilimali za umeme zilizopo pamoja na kupata umeme wa uhakika kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na katika Mkutano huu kila nchi imeonesha utayari kufanya biashara ya umeme pale kunapokuwa na umeme wa ziada.” Amesema Dkt. Biteko
Ameeleza kuwa kuna idadi kubwa ya watu katika nchi wanachama wa EAPP, hivyo inahitajika nishati zaidi kwa ajili ya maendeleo ya watu na viwanda na ndio maana kila nchi imejikita katika kuendeleza vyanzo mbalimbali vya umeme ajili ya kujipatia nishati ya uhakika.
Amesema kuwa, Tanzania itakuwa sehemu ya soko la umeme pale nchi jirani zitakapohitaji nishati hiyo, na hii ni baada ya kuwashwa kwa mashine zote Tisa katika Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere ambalo litazalisha megawati 2,115 ambazo zinatoa uhakika wa kutosheleza mahitaji ya ndani.
“Tanzania kuna njia mbalimbali za usafirishaji umeme (interconnectors) mfano Tanzania na Uganda, Tanzania na Burundi pamoja na Tanzania na Rwanda na sasa kuna laini ya umeme kutoka Tanzania hadi Kenya ambayo imekamilika na ipo kwenye majaribio itakayotuwezesha kufanya biashara kati ya nchi hizi mbili pale kila nchi ikiwa na umeme wa kutosha.”Amesema Dkt. Biteko
Ameongeza kuwa, kuna upembuzi yakinifu unafanyika chini ya Benki ya Dunia (WB) kwa ajili ya kujenga mradi mkubwa wa usafirishaji umeme wa msongo wa Kilovoti 400 kutoka Tanzania hadi Uganda kutokea Shinyanga, ambao utasafirisha umeme mwingi zaidi kwa baadhi ya mikoa kama vile Kagera na pia kuwezesha nchi hizo kufanya biashara ya umeme.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa, Sekta ya Nishati ni injini katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hivyo suala la kupeleka nishati ya kutosha, salama na ya gharama nafuu kwa wananchi si suala la hiari bali ni wajibu kwa ajili ya shughuli za uzalishaji na kijamii.
Ameeleza kuwa, ukuaji wa Sekta ya Nishati kwa nchi za Mashariki mwa Afrika ni asilimia 6 kwa mwaka, hivyo bado kuna kazi kubwa ili kuhakikisha wananchi katika nchi hizo wanapata nishati ya uhakika na kwa gharama nafuu.
Amesema chini ya mfumo wa pamoja wa umeme EAPP kuna miradi mbalimbali iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa kuimarisha upatikanaji wa nishati katika nchi wanachama akitolea mfano mradi wa ujenzi wa miundombinu ya umeme wa Kenya-Uganda, Kenya-Ethiopia, Kenya-Tanzania, Tanzania-Rwanda, Tanzania-Uganda, Tanzania-Burundi na DRC-Burundi.
Amesisitiza kuwa, nchi Wanachama zinapaswa kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili kupunguza changamoto za umeme kwani umeme huo utaweza kusafirishwa kutoka eneo moja kwenda jingine na kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika .
Awali, Mwenyekiti wa kikao hicho cha Baraza la Mawaziri wa Nishati ambaye ni Waziri wa Nishati na Petroli wa Kenya, Mhe. Davis Chirchir amesema lengo la nchi kuwa na mfumo huo ni nchi wanachama 13 kufanya biashara ya mauziano ya umeme pale kunapokuwa na ziada ya umeme, na kwamba ili suala hilo liwezekane lazima kuwepo na miumbombinu ya umeme inayounganisha nchi hizo.
Amesema kuwa, majadiliano ya viongozi hao yamelenga katika kuimarisha muundo wa umoja huo pamoja na ushirikiano na hii ikijumuisha namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za umeme pale zinapojitokeza.
Amesema Kenya tayari inafaidika na mfumo huo wa umeme baada ya kupokea magawati 200 za umeme kutoka nchini Ethiopia, hivyo kuongeza kiasi cha umeme katika nchi hiyo.
Ameongeza kuwa, takriban watu milioni 600 bado hawajapata nishati ya umeme barani Afrika kati ya watu takriban Bilioni 1.5 na hii ikionesha jinsi nguvu zaidi inavyohitajika ili kuwa na nishati ya kutosha kuweza kukidhi mahitaji.
Nchi Wanachama wa Umoja wa EAPP ni pamoja na Kenya, Tanzania, Sudan Kusini, Sudan, Uganda, Somalia, Libya, Ethiopia, Misri, Djibouti, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Wadau wa Maendeleo ikiwemo Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB).
Viongozi wengine wanaoshiriki Mkutano huo kutoka Tanzania ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima-Nyamohanga.
More Stories
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais
NIDA yawakumbusha wananchi kuchukua vitambulisho vyao