January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Eagle Entertainment Awards yatoa tuzo 22, kutambua mchango wa watu mbalimbali

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Sengerema

Jumla ya tuzo 22 katika vipengele mbalimbali zimetolewa na Eagle Entertainment Awards katika usiku wa tuzo msimu wa mwaka 2022 wilayani Sengerema mkoani Mwanza.

Huku wito ukitolewa kwa wasanii wilayani humo kufanya kazi kwa bidii, kuwa na heshima kwa jamii pamoja na kutumia sanaa yao kuzuia mmomonyoko wa maadili katika jamii huku serikali ikiwaunga mkono.

Tuzo hizo ambazo zimefanyika usiku wa kuamkia Desemba 26,2022 ikiwa ni mara ya pili ambapo mara ya kwanza zilifanyika mwaka na 2021 ambazo zimeandaliwa na Eagle Entertainment Awards.

Katika tuzo hizo kwa msimu huo wa pili vipengele mbalimbali viliwaniwa ikiwemo msanii bora wa kike,msanii bora wa kiume,wimbo bora wa mwaka,mwandishi bora wa gazeti,mtangazaji bora wa radio,mpiga picha bora, Dj bora, mshereheshaji bora,mpambaji bora wa harusi, kikundi bora cha ujasiriamali, mzalishaji bora wa filamu pamoja na tuzo za heshima.

Akizungumza mara baada ya zoezi la utoaji wa tuzo,muaandaaji wa tuzo hizo,Mkurugenzi wa Eagle Entertainment na Ngoko TV, Hassan Kuku,
ameiomba serikali kutambua mchango wa wasanii wanaochipukia kwa lengo la kuwafanya wawe wasanii wakubwa siku za usoni.

“Usiku huu wa tuzo tumefanya kwa ajili ya kutambua mchango wa watu katika sekta na tasnia mbalimbali ili kuwaongezea thamani kwa watu wanaofanya shughuli mbalimbali za kisanaa,ujasiriamali na kiburudani,ili watu waamini kuwa vipaji vyao vinaweza kuwasogeza mbali,lengo la tuzo hizo ni watu kutambua thamani yao na kuwaongezea thamani wao kwa kile walichokifanya,”ameeleza Kuku.

Pia Kuku,ameiomba Serikali iendelee kuwasaidia vijana katika nyanja mbalimbali sababu vijana wengi wanavitu vya kufanya lakini uungwaji mkono unakuwa ni ndogo.

Ameeleza kuwa una watu wana vipaji vikubwa vinavyoweza kuwasogeza sehemu fulani lakini vinapotea kwa sababu hawana mtu wa kuwasaidia kwa kuwaunga mkono.

“Katika Halmashauri yetu ya Wilaya ya Sengerema kuna mikopo inayotolewa ile ya Halmashauri lakini elimu inayotoka ni ndogo ya kuelimisha vijana kuhusiana na fedha hizo za mikopo ambayo serikali imewekeza,pia serikali itusaidie katika miradi ‘project’ kama hiyo kwani itakuwa imesaidia kundi kubwa la vijana na jamii kwa ujumla,”ameeleza Kuku.

Sanjari na hayo ametoa rai kwa vijana kuwa wabunifu pamoja na kufanya mambo mengi ya kimaendeleo kwani wengi wao wamejikita katika kukwamisha watu wengine ambao wana mlengo chanya wa kufanya vizuri.

“Vijana tujifunze kupitia kwa wengine waliofanikiwa ili na sisi tusogee pale walipo fanikiwa,”.
Akizungumzia suala la tuzo Kuku ameeleza kuwa kwa Sengerema uelewa wa tuzo hizo bado upo chini kwa sababu ni kitu kipya ambacho wamezoea kuona katika maeneo mengine hasa wamezoea kuona tuzo zikifanywa na watu wakubwa nchini

“Katika tuzo hizi tulikuwa na vipengele 18 na tuzo nne za heshima jumla tumetoa tuzo 22, changamoto ni kuwa tuzo zinahitaji pesa hivyo tunaomba wadau waweze kutuunga mkono na sisi tupo tayari kuwapokea,”.

Mshindi wa tuzo ya mtangazaji bora kutoka Radio Sengerema Said Mahela, ameeleza kuwa tuzo hizo ni chachu kwa watangazaji katika shughuli zao na kwa upande wake zitamsukuma kwenda mbele na kuwa chachu kwa vijana kuwabadilisha katika maadili mabaya na kuwa wema.

Naye Lyidia Juakali maarufu De amber ambaye amejinyakulia tuzo mbili ikiwemo ya msanii bora wa kike na wimbo bora wa mwaka, ameeleza kuwa Wilaya yao imekuwa na uhaba wa wasanii wa kike hivyo kupitia yeye anaimani watajitokeza wengi.

“Watoto wa kike tunaputia changamoto nyingi sana katika sanaa,ni mara yangu ya kwanza kushiriki katika tuzo hizi,watoto wa kike wanakwamishwa na rushwa ya ngono hivyo maproducer mtoto wa kike akija kufanya kazi kwako muache afanye kazi kwani Sanaa ni kazi kama zilivyo nyingine,”

Kwa upande wake Mgeni rasmi katika tuzo hizo Diwani wa Kata ya Tabaruka Sospeter Busumabu,amewataka washiriki wa tuzo hizo na vijana kwa ujumla kuwa na nidhamu katika kazi zao pamoja na kuheshimi wote wanaofanya nao kazi.

“Mimi bila Sanaa nisinge soma shule,nilipoenda shule kwa sababu ya sanaa,sanaa ni maisha hata harusi haiwezi kufanyika kama hamna sanaa mziki, tupambane kuhakikisha kwamba tunaboresha Sanaa katika Wilaya yetu twende mbali zaidi Sengerema siyo ya kukosa wasanii wakubwa, na alichokianzisha Hassan Kuku tumuunge mkono,”ameeleza Busumabu.

Baadhi ya watu waliojinyakulia tuzo ni pamoja na Daniel Makaka mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi,alipata tuzo ya mwandishi bora wa gazeti,huku tuzo za heshima zikienda kwa Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Mbunge wa Jimbo la Sengerema na wengineo.

Mkurugenzi wa Eagle Entertainment na Ngoko TV, Hassan Kuku, akizungumza katika usiku wa tuzo kwa mwaka 2022, Wilaya ya Sengerema ambazo zimetolewa na kuaandaliwa na Eagle Entertainment Awards.
Baadhi ya wadau mbalimbali wa burudani wilayani Sengerema waliohudhuria usiku wa tuzo,ambapo tuzo 22 zilitolewa kwa watu mbalimbali ikiwemo wasanii, wajasiliamali iliondaliwa na Eagle Entertainment Awards.
Mwandishi wa habari mkoani Mwanza Mariam John akimkabidhi tuzo Said Mahela mtangazaji wa radio Sengerema aliejinyakulia tuzo ya mtangazaji bora Wilaya ya Sengerema, iliofanyika usiku wa kuamkia Desemba 26,2022 wilayani humo mkoani Mwanza na kuaandaliwa na Eagle Entertainment Awards.