January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DUWASA kutumia shilingi Bilioni 9.5 kukarabati na kuchimba Visima pembezoni mwa Jiji

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

MKURUGENZI wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma(DUWASA)Mhandisi ,Aron Joseph amesema Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 9.5 kwa mwaka wa fedha 2022/23 kwajili ya ukarabati na uchimbaji wa Visima pembezoni mwa Jiji la Dodoma.

Mha.Joseph amesema hayo jijini hapa leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli za DUWASA na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2022/23

Ambapo amevitaja vyanzo hivyo vilivyopo maeneo ya pembezoni mwa Jiji kuwa ni  Zuzu, Ihumwa, Mpunguzi, Nala, Michese, Zinje na Nzuguni.

“kwa sasa Jiji la Dodoma lina takwimu zifuatazo kuwa dadi ya Wakazi ni 500,000 ambao wanapata maji safi ni asilimia 82,
mahitaji ya maji ni lita milioni 133 kwa siku hii ni kwa mwaka 2022 na yataongezeka hadi lita milioni 204 kwa siku hadi ifikapo mwaka  2036,Uwezo wa kuzalisha maji ni lita milioni 67.1 kwa siku kituo cha Makutupola pekee ni  lita milioni 61.5,huku vituo vingine vikizalisha lita milioni 5.6 sawa na asilimia 50ya mahitaji ambapo muda wa kutoa huduma ni wastani wa saa 10 kwa siku,”amefafanua Mha.Joseph.

Akizungumzia mipango inayopewa kipaumbele katika mwaka wa fedha 2022/23 amesema kwa  upande wa maji safi DUWASA kwa kushirikiana na Wizara ya Maji imeendelea na utafiti wa namna bora ya kuendana na kasi ya mahitaji, kwa kubuni mbinu mbalimbali za utatuzi wa changamoto ya uhaba wa majisafi na uondoshaji Majitaka kwa kuanzisha utekelezaji wa mipango ya dharura, muda mfupi, kati na mrefu ili kuongeza kiasi cha upatikanaji wa maji kwa ajili ya Jiji la Dodoma.

Ametaja mipango hiyo kuwa ni Mpango wa Dharura na Muda Mfupi, Ujenzi wa Mradi wa kutoa maji Bwawa la Mtera ambapo Chanzo kipo tayari ambacho kitakamilishwa kati ya miaka 2 hadi 2.5 huku Benki ya Dunia ikiwa tayari kufadhili gharama ya Mradi ni Dola milioni 140 sawa na bilioni 326 za Tanzania.

Aidha amesema mradi huo utaongeza maji lita milioni 130 kwa siku pia utaongeza mtandao wa usambazaji maji katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na kuondoa migao ya mamaji.a

Kwa upande wa  fedha za Mpango wa Maendeleo na Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19,Mha.Joseph amesema DUWASA kupitia Wizara ya Maji ilipokea kiasi cha shilingi Bilioni 1.1 huku mradi wa Ntyuka Chimalaa ukikamilika kwa asilimia 100,Bahi town kwa asilimia 100
na uchimbaji wa visima 6 kwa asilimia 100 huku jumla ya wanufaika wakiwa 40,000.

“Kuna mpango wa muda wa Kati na Mrefu ambao ni ujenzi wa Bwawa la Farkwa ukiwa na muda wa mradi miaka 5 hadi 6 na
Ongezeko la maji mita milioni 128 kwa siku gharama ya mradi ikiwa Dola milioni 135.8 sawa na shilingi bilioni 312.08 za Tanzania,

“Tarehe 16/05/2022 Serikali ya Tanzania ilisaini financial agreement na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ya Dola mil. 125.3 (shilingi Bilioni 289) kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa pamoja na Chujio (treatment plant) na mpaka sasa tayari Mhandisi Mshauri amepatikana na anatarajiwa kusaini mkataba mwezi Agosti mwaka huu,”ameeleza.

Kwenye usafi wa mazingira (majitaka),Mha.Joseph amesema Mradi wa uboreshaji wa huduma ya Majitaka jijini dodoma unaofadhiliwa na Serikali ya Korea kupitia mkopo wa Masharti nafuu,ambao unalenga kuhudumia kata 11 na kuboresha mtandao uliopo katika kata 14.

Amesema mradi huo utaweza kutibu majitaka lita milioni 20 kwa siku,utahusisha ujenzi wa mabwa 16 eneo la Nzuguni, Utaongeza mtandao wa majitaka usiopungua kilomita 250,utaunganisha wateja wasiopungua 6,000 na kuongeza huduma ya usafi wa Mazingira kutoka asilimia 20 hadi 45.

Ameeleza kuwa Mradi huo una gharama ya shilingi bilioni 161 na sasa upo katika hatua za mwisho za kumpata Mkandarasi Mshauri.

“Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kushirikiana na DUWASA ipo katika hatua za mwisho kusaini mkataba na Mhandisi Mshauri na Mradi wa maji katika mji wa kiserikali ambao unatarajiwa kugharimu takribani shilingi za Tanzania Bil. 94, ambazo zimeshatengwa na Serikali Kuu,”amesema.

Pamoja na hayo Mkurugenzi huyo alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha Wananchi wa Dodoma kutunza miundombinu ya majisafi na majitaka lakini pia kutunza vyanzo vya maji kwa kuboresha mazingira hasa upandaji na utunzaji wa miti.