January 17, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dube kutua nchini kesho, aandaliwa programu maalum

Na Mwandishi Wetu

MSHAMBULIAJI wa kikosi cha Azam FC Prince Dube anatarajiwa kutua hapa nchini kesho usiku akitokea nchini Afrika Kusini alipokwekwa kwa ajili ya upasuaji wa mkono baada ya kuvunjika mfupa wa mbele wa mkono wake wa kushoto unaoitwa Ulnar.

Kinara huyo wa mabao ndani ya Azam FC aliumia dakika ya 15 ya mchezo wao wa Novemba 25 dhidi ya Yanga ambao walikubali kichapo cha goli 1-0 katika uwanja wao wa nyumbani wa Azam Complex na kushushwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL).

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa klabu hiyo, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ amesema, baada ya upasuaji wake kwenda sawa, nyota huyo atatua hapa nchini kesho usiku na kuendelea na matibabu huku akiendelea kupona taratibu.

Wakati akiendelea na matibabu hayo pia atakuwa katika programu maalum ya mazoezi ya peke yake kwani licha ya kuumia mkono, kocha wa viongo wa timu hiyo Nyasha Chalandula amependekeza kuendelea na mazoezi madogo ya peke yake.

Chalandula amejiunga na Azam siku chache zilizopita akitokea ndani ya kikosi cha timu ya Taifa ya Zimbabwe.

Majeruhi wengine ndani ya kikosi hicho, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Abdallah Heri ‘Sebo’ wanaendelea vizuri lakini wataendelea kuukosa mchezo wao wao wa Desemba 14 dhidi ya Namungo.