January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dua ya kumuombea Rais Samia yatikisa Mkuranga

*Ni kwa uongozi wake kuendelea kudumisha utulivu na amani,

*Yashirikisha waumini wa kiislam, kikiristo, Mawaziri na Manaibu Waziri

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online, Pwani

KIU ya kuimarika kwa amani, usalama na utulivu nchini, imewakutanisha maelfu ya waumini wa dini ya Kiislamu na Kikristo kutoka ndani na nje ya wilaya Mkuranga, mkoani Pwani kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan na taifa ili lizidi kuwa na mshikamano.

Dua hiyo iliyoandaliwa na Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega akishirikiana na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA)wilayani Mkuranga,ambayo imefanyika Desemba 14,2024,uwanja wa shule ya msingi Mkuranga mkoani Pwani.

Dua hiyo ilitanguliwa na Maulid ya Mtume Muhammad (S.A.W) yaliyofanyika asubuhi na kuwakutanisha masheikh mbalimbali waandamizi wakiwemo wa Mikoa ya Arusha, Kigoma, Kagera, Dar es Salaam na Pwani.

Maulid hayo yalibeba kauli mbiu isemayo,”Tulinde maadili yetu,amani yetu kwa maslahi ya Taifa letu”,ambapo Watanzania wamesisitiziwa kuitunza na kuimarisha amani iliyopo ,ili kuunga mkono jitahada za Rais Samia ambaye amekuwa mstari wa mbele kuihubiri.

Watanzania wameomba kuitunza amani na utulivu katika kipindi chakuelekea kufunga mwaka 2024 na kuingia mwaka 2025, ambapo Tanzania itafanya uchaguzi wake mkuu wa kumchagua Rais,Wabunge na Madiwani.

Imeshuhudiwa kwa nyakati tofauti kumekuwa na matukio ya mmomonyoko wa maadili ambapo Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kukemea na kuwataka viongozi wa dini kuungana na Serikali katika kusimamia suala hilo.

Wengine ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deo Ndenjembi na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, pia walikuwepo mameya, wakurugenzi na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge.

Akitoa nasaha maalumu katika dua hiyo, Sheikh wa Mkoa wa Arusha, Shaaban Juma, amesema kongamano hilo lililoambatana na dua lina tafsiri nyingi ikiwemo kutoa maelezo au ishara kwamba amani imetawala.

” Nchi isiyokuwa na amani, mkusanyiko kama huu wa kumswalia Mtume Muhammad, kumuombea dua Rais wetu na Taifa kwa ujumla inakuwa ni vigumu, lakini Tanzania tumebarikiwa kuwa amani tuilinde na kuitunza,”amesema na kuongeza:

” Mali au fedha unaweza ukazificha mfuko au mahali pengine, lakini binadamu utamficha wapi asione na shari au dhuluma?.Amani ndio kila kitu ndugu zangu, tuitunze, namshukuru Ulega na wenzake kufanya tukio kama hili, muda tungekuwa tumelala lakini tupo hapa sasa hivi ( saa tano usiku),”

Akizungumza kwa niaba ya Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir, Mjumbe wa Baraza la Ulamaa la Bakwata Sheikh Himid Jongo amempongeza Ulega kwa kuandaa tukio muhimu ambapo Watanzania wamepata fursa ya kuombea Rais Samia na Taifa kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, Sheikh Jongo alitumia nafasi hiyo kumuomba Ulega kushughulikia changamoto ya ufinyu wa barabara eneo la Mto Mzinga Mbagala akisema limekuwa kero kwa muda mrefu.

Naye, Waziri wa Ujenzi ,Abdallah Ulega alianza kwa kumshukuru MuRais Samia kwa kuendelea kumuamini huku akiahidi kutomuangusha katika utekelezaji wa majukumu yake mapya ya sekta ya ujenzi.

“Umati huu umetoka katika vijiji vyote vya kata 25 za wilaya ya Mkuranga,tumejiwekea malengo pia ya kuboresha huduma za jamii zetu,” amesema Ulega.

Kwa upande wake,Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge,amesema Rais Samia amefanikiwa kuweka mazingira mazuri ya amani katika maeneo mbalimbali ndiyo maana tukio hilo limefanikiwa kwa dini tofauti kujumuika na kufanya ibada.

“Tuombe kwa Mungu amzidishie afya njema Rais Samia, umri mrefu, subira na uvumilivu,” amesema Kunenge.

Mkazi wa Kata ya Kisiju, Mohamed Mperi, “hili ni tukio adhimu linalokutanisha wananchi mbalimbali kwa ajili ya dua maalumu.Tukio hili yanasaidia kujuana kukutana na kutoa mafundisho ya upendo wa watu kupendana na kubadilishana mawazo,” amesema Mperi.

Miongoni mwa mawaziri waliokuwepo ni Jumaa Aweso( Waziri wa Maji) na Ridhiwani Kikwete ( Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, ajira na Watu wenye Ulemavu) wawili hawa walikuwa kivutioa kwa kuimba Qaswida kwa umahiri.