November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Philip Fumbo akitoa neno la shukrani mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu

DP yatambulisha rasmi wagombea wa Urais Tanzania na Zanzibar

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma

CHAMA cha Demokratic (DP) kimemteua Philip Fumbo kuwa mgombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika oktoba 28 mwaka huu kupitia chama hicho huku kikijitanabaisha kwamba kinakwenda kushinda.

Katibu Mkuu wa DP Abdul Mluya

Chama hicho pia kimewateua Shaffii Hasssan Suleiman kuwa mgombea Urais Zanzibar na Zaina Juma Khamis kuwa mgombea mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza leo jijini Dodoma na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama hicho Katibu Mkuu wa DP, Abdul Mluya amesema chama kimewachagua wagombea hao kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu kwani kinawaamini na kwamba kinakwenda kushinda na kushika dola.

Mluya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Uchaguzi wa chama hicho katika mkutano huo amekiri kuwa mgombea wao wa urais ana kazi kubwa katika mapambano ya kinyang’anyiro cha kiti cha urais dhidi ya Rais anayemaliza muda wake kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) John Magufuli.

“Mkutano Mkuu umemteua Philip Fumbo kwenda kuminyana na Magufuli, ingawa kuna ugumu kwani Magufuli anatetea kiti chake, lakini tutabanana naye hivyo hivyo, Philip siyo mtu wa kubeza, haendi kutania,” amesema Fumbo

Mluya ametumia fursa hiyo kuiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iwatangaze pindi watakapopata ushindi na kwamba wao wapo tayari kumpa hongera mshindi atakayepata ushindi huo kihalali.

Mgombea urais Zanzibar Shaffii Hussein Suleiman akitoa neno la shukrani kwa wajumbe

“Watu huwa wanasema sisi tunapenda kesi, hili tunasema kweli kwamba tupo tayari kufungua kesi hata elfu kumi kama hatutatendewa haki .”amesema Mluya

Kwa upande wake Fumbo amesema, kutokana na sera nzuri ya walala hoi katika ilani yao ambayo inakwenda kuwapa ushindi kwani Watanzania wengi ni walala hoi.

Naye mgombea Urais wa Zanzibar, Suleiman amesema akipata nafasi ya kuwatumikia Watanzania kwa upande wa Zanzibar atakwenda kutatua changamoto nyingi zinazowakabili Wazanzibar kwa kutumia rasilimali nyingi walizonazo ikiwemo bahari.