Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Hospitali ya Taifa Muhimbili imekabidhiwa msaada wa taulo za watoto wachanga aina ya Softcare zenye thamani ya TZS. 35Mil kutoka kampuni ya DOWEICARE ili kusaidia watoto waliozaliwa na watakaozaliwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia sasa.
Akipokea msaada huo kwa niaba ya Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mh. Albert Chalamila ameipongeza DOWEICARE kwa mchango huo ambao utasaidia kina mama na watoto wao hasa wasio na uwezo wa kumudu kununua taulo hizo mara tu wanapojariwa kupata baraka za watoto.
“DOWEICARE mmeonesha kujali kwani taulo hizi zitasaidia katika kutunza na kuandaa afya ya mtoto ambaye siku za usoni atakuwa kiongozi mwenye mawazo chanya na akili njema itakayotumika katika kuliongoza taifa letu kwani mara nyingi tumekuwa tukitoa msaada kwa watu wazima na kusahau kuwa watoto ni watu muhimu katika jamii hasa katika kuandaa taifa imara na bora lenye maendeleo makubwa,” amesema Mh. Chalamila.
Akipokea msaada huo Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi ameishukuru kampuni hiyo na kuwaomba kuendelea kuunga mkono hospitali kutokana na kuhudumia wagonjwa wengi na wenye vipato tofauti.
“Tunajua nyie niwatengenezaji wa bidhaa muhimu ambazo tunahitaji zaidi katika kuwahudumia watoto hivyo ombi letu kwenu ni kuwa tunaomba hapo baadaye mtuuzie bidhaa hizi kwa bei ya punguzo kwani kufanya hivyo mtakuwa mmewasaidia watoto wachanga wanaozaliwa na kuhudumiwa hospitalini hapa,” amesema Prof. Mohamed.
Akikabidhi msaada huo Mkurugenzi Mtendaji wa DOWEICARE Bw. Victor Zhang amesema kuwa wanatambua mchango mkubwa unaotolewa na Hospitali hii hivyo wataendelea kushirikiana ili kuboresha huduma za afya katika maeneo kadhaa.
Naye Balozi wa Softcare nchini Bi. Zarina Hassan maarufu “Zari the Boss Lady” ametaka jamii kutambua umuhimu kwa kuitunza afya ya mtoto kwa kutumia bidhaa zenye ubora na kusema kuwa taulo za Softcare zina ubora wa hali ya juu na salama kwa watoto wachanga.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi