Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
BARAZA jipya la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya limefanya uchaguzi wa viongozi wake ambapo Diwani wa Kata ya Isanga, Dour Issah Mohamed amechaguliwa kuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya baada ya kupata kura 48 kati ya 49 sawa na asilimia 98.
Katika uchaguzi huo, Diwani wa Kata ya Iziwa, Kefas Mwasote, amechaguliwa kuwa Naibu Meya baada ya kupata kura zote 49 akishinda kwa asilimia 100.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi Desemba 5, 2025, Mstahiki Meya Mohamed ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na madiwani wote bila kujali tofauti zao za kisiasa au uchaguzi.
Amesisitiza kuwa yeye ni binadamu asiye mkamilifu, hivyo ni muhimu kwa viongozi na watendaji kufanya kazi kwa upendo na kuheshimiana.
“Milango yangu iko wazi, nyumbani na ofisini. Sitapokea majungu ya aina yoyote,”amesema.
Ameongeza kuwa kamati zitakazoundwa ndani ya baraza hilo ni za muda na hazipaswi kuwa chanzo cha mgawanyiko, akiwataka wajumbe wote watakaoteuliwa kufanya kazi kwa uadilifu ili Jiji la Mbeya liwe mfano bora nchini.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbeya, Mohamed Fakii amewashauri madiwani na wataalamu wa halmashauri kufanya kazi kwa uadilifu, kutatua kero za wananchi kwa ushirikiano, na kusimamia kwa karibu mapato ya jiji.
Amesisitiza pia umuhimu wa kufuatilia na kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa kwenye hotuba za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hususan yanayolenga ustawi wa vijana na maendeleo ya wananchi.
“Mbeya iko salama. Mtu yeyote mwenye kero awasilishe sehemu husika,” ameongeza.
Akitoa neno la shukrani, Naibu Meya wa Jiji la Mbeya, Kefas Mwasote, ameahidi kushirikiana kikamilifu na wataalamu pamoja na madiwani wote katika kutekeleza majukumu ya jiji hilo.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi