November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Doria za kudhibiti wanyamapori wakali, waharibifu zatarajiwa kuimarika

Na Penina Malundo, timesmajira

WIZARA ya Maliasili na Utalii inamatarajio makubwa ya kuimarika kwa shughuli za doria za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu na hivyo kupunguza migongano baina ya binadamu na wanyamapori.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamisha wa Polisi (CP) Benedict Wakulyamba alipokuwa akifunga mafunzo maalum kwa Askari Wahifadhi toka TAWA na kozi Na. 73/2024 kwa Askari Wanyamapori wa Vijiji (VGS) katika Chuo cha Likuyu Sekamaganga Wilaya ya Namtumbo Mkoa wa Ruvuma.

CP Wakulyamba amesema wananchi wanapaswa kuzingatia maelekezo yanayaotolewa na wataalamu wa taasisi za uhifadhi ili kuepuka madhara ya wanyamapori wakali na waharibifu, kuzingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo yaliyopo jirani na hifadhi, mapito na mtawanyiko wa wanyamapori.

Amesema wananchi hao wanapaswa kujiepusha na tabia ya kupiga wanyamapori wakali kwa kutumia silaha mbalimbali za kimila/jadi pindi wanapoingia kwenye maeneo ya wananchini.

“Takribani Askari wanyamapori 150 wamehitimu fani ya uwaskari wa Wanyamapori,katika kuongeza ufanisi utatuzi wa Migogoro ya kuhifadhi,”amesema.

Ametaja matarajio mengine ya Wizara kwa wahitimu hao ni pamoja na kuongezeka kwa ufanisi wa kuitikia kwa haraka kwenye matukio kutokana na kuwa, VGS mnaohitimu mtakuwa kwenye maeneo yenye changamoto na hivyo kuwa mstari wa mbele katika kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu kabla hawajasababisha Mathara.

Licha ya kuwapongeza wahitimu hao, CP Wakulyamba amekipongeza Chuo Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii-Likuyu Sekamaganga, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa kuendelea na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kitaifa wa kutatua changamoto za muingiliano baina ya binadamu na Wanyamapori wa mwaka 2020 hadi 2024.

Akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa cha Uhifadhi wa Vijiji kwa Jamii Likuyu Sekamaganga,Jane Nyau ameeleza jumla ya Askari Wahifadhi 28 toka kwenye Mapori ya Akiba ya Selous na Liparamba na VGS 122 kutoka Wilaya 34 wamehudhuria mafunzo haya.

Naye Mkurugenzi wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo Dkt. Edward Kohi amesema Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia vyuo vyake vya mafunzo itaendelea kutoa Mafunzo mbalimbali ya Uhifadhi kwa kuwajengea uwezo Askari wa Jeshi la Uhifadhi pamoja na Askari wa Wanyamapori wa Vijiji ili kuimarisha Shughuli za Uhifadhi kwa kushirikiana na wanavijiji waishio jirani na Hifadhi.

Msimamizi Mkuu wa Mradi wa Frankfurt Zoological Society,Kathryn Doody licha ya kuipongeza Serikali kwa kuendesha Mafunzo kwa askari wa Jeshi la Uhifadhi na VGS, amewakumbusha askari hao kutambua kuwa kazi wanayofanya ni muhimu sana, siyo kwa Tanzania tu bali kwa ulimwengu wote.