May 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Doreen: ‘Msiwafiche watoto wenye utindio wa Ubongo

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

JAMII imetakiwa kutokuwaficha watoto wenye utindio wa ubongo kwani ni watoto kama walivyo wengine.

Wito huo umetolewa na Doreen Fitzpatrick ambaye ni Mtanzania anayeishi Marekani na Mkurugenzi wa Sassyfly Luxury Event wakati akitoa msaada katika Kituo cha kulelea watoto wenye Utindio wa Ubongo cha Dorcas Homecare Initiative kilichopo Madale, jijini Dar es Salaam.

Akikabidhi msaada huo ambao ni viti saba vya walemavu (wheelchair), diapers pamoja na vyakula mbalimbali, Doreen amesema ameamua kuja Tanzania ili kurudisha shukrani kwa jamii.

“Watoto wenye mtindio wa Ubongo ni watoto kama watoto wengine hivyo wazazi wasiwafiche watoto hao bali wawapeleke katika vituo maalum ili wafundishwe stadi mbalimbali za maisha.

“Nimekuwa nje ya nchi kwa miaka 10, kwahiyo nimerudi Tanzania kurudisha kwa jamii yangu. Na katika kufikiria kitu cha kufanya nikaona ni bora niwasaidia watoto hawa…tunajua kuna vituo vya watoto yatima lakini sio wengi wanajua kuhusu utindio wa Ubongo,” amesema Doreen.

Akipokea msaada huo, Rehema Semfukwe amemshukuru Doreen kwa kuona umuhimu wa kuwasaidia kwani unaonyesha moyo wa upendo kwa watoto hao wenye mahitaji maalum.

“Tunamshukuru Doreen kwa msaada huu mkubwa, na tunaomba wengine nao wajitokeze waweze kutusapoti katika mambo mbalimbali ikiwemo kupata usafiri wa kuwachukua watoto majumbani mwao kuwaleta hapa kituoni na kuwarudisha,” amesema Rehema.

Amesema Kituo hicho kina jumla ya watoto 15 na wengi wao wanatokea eneo hilo la Madale ambapo asilimia 99 hawawezi kufanya chochote ikiwemo kutembea na kuongea.

“Mungu ametupa maono haya ya kuanzisha Dorcas Homecare Initiative baada ya mimi kupata mtoto mwenye utindio wa ubongo. Kwahiyo kutokana na nimemlea mtoto wa aina hii na kuona changamoto ambazo nimekutana nazo na nikaweza kujua ni kwa namna gani wazazi wengine wanapitia hali kama hii ambayo mimi nimepitia.

“Na hapa watoto wanapata mazoezi ya viungo na lishe kuanzia asubuhi mpaka jioni halafu wanarudi nyumbani…tuliamua kuwachukua na kuwarudisha tuliamini kuna muda wanahitaji kukaa na wazazi wao,” amesema.

“Kuna watoto wengi kwenye jamii wanapitia changamoto kama hii lakini kuna wazazi wamekosa ujasiri wakusema changamoto za watoto wao. Kwahiyo sisi tunapaza sauti kwa niaba yao.

“Lengo lingine la kuanzisha Kituo hiki ni kuwasaidia wazazi kwani unapokaa na mtoto wa aina hii masaa 11 unamsaidia mzazi aweze kufanya chochote cha kumuingizia kipato,” amesema.

Akielezea kuhusu Utindio wa Ubongo, Mtaalamu wa Tiba na mazoezi ya Viungo, Ismail Makoye amesema Utindio wa ubongo au Cerebral Palsy ni tatizo la ubongo ambalo huathiri watoto na husababishwa wakati damu inapovuja kwenye ubongo.

“Kuna aina tofauti za utindio wa ubongo lakini inayofahamika zaidi ni Spastic cerebral palsy ambayo husababisha viungo na misuli kuganda. Hali hii humfanya mtoto kuwa na uchungu mwingi na mifupa hushindwa kulainika hivyo huchukua muda kabla ya mtoto kutembea,” amesema.