NEW YORK, Umoja wa Mataifa umetoa dola milioni 135 kutoka kwenye Mfuko wake wa Dharura (CERF) ili kuongezea kwenye shughuli za kibinaadamu katika nchi 12 barani Afrika, Amerika na Mashariki ya Kati.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa Mfuko huo, Mark Lowcock akiwa mjini New York nchini Marekani.
Amesema, fedha hizo zimetolewa kufuatia takwimu zilizotolewa wiki iliyopita, zikionesha zaidi ya watu 350,000 wanakabiliwa na njaa katika mji wa Tigray Ethiopia, na tishio la njaa katika nchi ya Burkina Faso, Kusini mwa Madagascar, Kaskasini-Mashariki mwa Nigeria, Sudan Kusini na Yemen.
“Njaa inaendelea kuongezeka maeneo kadhaa hivi sasa, mgawanyo huu wa fedha zilizotolewa unaweza kuleta tofauti kati ya maisha na kifo, kwa mamilioni ya watu wanaotegemea msaada ili kuishi. Msaada utatoa vitu muhimu kama maji safi, malazi na chakula kwa watu walio na uhitaji sana wakati huu,”amesema.
Ameeleza kuwa, fedha hizo zitagawanywa kwenye mashirika ya misaada ambapo Syria itapata dola milioni 20, Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC) dola milioni 20, Ethiopia zilielekezwa mkoa wa Tigray dola milioni 13.
Nchi za Afghanistan, Nigeria na Sudan Kusini kila moja itapata dola milioni 11 kusaidia shughuli za misaada. Na fedha zilizosalia zitapelekwa Madagascar dola milioni 8, Venezuelea dola milioni 7, Chad dola milioni 7, Burkina Faso dola Milioni 7, Cameroon dola Milioni 5, na Msumbiji dola milioni 5.
Miradi ya kusaidia watu wenye ulemavu imetengewa dola milioni 10. “Mahitaji ya kibinadamu yanaendelea kuzidi misaada ya kibinadamu inayotolewa, na sio mizozo yote inayopewa uangalifu sawa wa uhitaji wa kifedha, na ndio maana mfuko huu kwa sasa ni muhimu kupita wakati mwingine wowote sababu unakuwa nyenzo muhimu ya kurekebisha usawa kwa kuhakikisha kuwa kazi muhimu ya misaada inaendelea kila mahali,”amesema Lockcock.
Tangu kuanzishwa kwa mfuko huo wa dharura mwaka 2005 ambao unapokea mchango wa hiyari kutoka nchi 129 pamoja na wadau wengine wa misaada, mamilioni ya watu wamepata msaada wa dola za Kimarekani bilioni 7 kwenye zaidi ya nchi 100 duniani, hii ikijumlisha zaidi ya dola bilioni 2.3 kwenye mizozo iliyopata ufadhili kidogo tofauti na uhitaji wake.
More Stories
Prof.Muhongo kufanya mkutano wa dharura kujadili ufunguzi Sekondari ya Nyasaungu
Bilioni 8.6, kutumika kwa ruzuku nishati safi ya kupikia
Waipongeza Serikali miradi ya zaidi ya tirioni moja