December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DMI yaomba miundombinu yake ikarabatiwe

 Meja Jenerali mstaafu, Said Shaaban ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) akizungumza wakati wa kusanyiko la wahitimu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), lililofanyika chuoni hapo Posta Dar es Saklaam.
 Baadhi ya washiriki wa kusanyiko la wahitimu wa DMI wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa na wataalamu wa chuo hicho kuelekea mahafali yanayofanyika siku ya Alhamisi chuoni hapo.
 Mgeni rasmi Meja Jenerali mstaafu, Said Shaaban ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) akiwa kwenye picha ya pamoja na kamati ya maandalizi ya kusanyiko la wahitimu wa DMI
Mgeni rasmi Meja Jenerali mstaafu, Said Shaaban ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) akiwa kwenye picha ya pamoja na wanafunzi wa  Chuo cha Bahari DMI waliofanya vizuri kwenye masomo yao.
 Mgeni rasmi Meja Jenerali mstaafu, Said Shaaban ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) akiwa kwenye picha ya pamoja nawafanyakazi wa DMI

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

CHUO cha Bahari Dar es Salaam, (DMI), kimeomba serikali ikipatie meli ya mafunzo kwaajili ya kuwaongezea ujuzi wahimu wa mafunzo chuoni hapo na kimeomba miundombinu ya chuo hicho ikarabatiwe ili kwenda na wakati.

Ombi hilo limetolewa na Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Dk. Tumaini Gurumo wakati akizungumza kwenye kusanyiko la wahitimu wa chuo hicho ambalo limefanyika chuoni hapo Posta Dar es Salaam.

“Uzuri wa meli ya mafunzo inakuwa imetengenezwa maalum kwaajili ya mafunzo, inakuwa na madarasa na vyumba vya kulala mle na unaweza kuifanya ya biashara ukaingiza fedha na wakati huo huo ya mafunzo hivyo uendeshaji wake ukawa rahisi kidogo kwasababu kumiliki meli siyo rahisi sana

“Kwa hiyo tukipata meli ya aina hiyo hata kama itakuwa inasafirisha kontena kutoka Tanzania kwenda nchi zingine itasaidia kupata nafasi za mafunzo kwa wanafunzi wetu na hivyo kupata mabaharia wengi sana hapa nchini,” amesema

 Aidha, Dk. Tumaini amesema mahitaji ya mabaharia ni makubwa sana lakini wengi wanaohitimu mafunzo ya nadharia wako mitaani wakisubiri kupata mafunzo ya vitendo ili waweze kukamilika.

Ametaja changamoto inayokabili chuo hicho kuwa ni uchakavu wa miundombinu kwani kimekuwa kikitumia miundombinu ile ile ya miaka ya 80 tangu kianzishwe kikiwa na wanafunzi 12 na inaendelea na miundombinu hiyo hiyo kikiwa na wanafunzi 4,049.

“Kwa hadhi ya wataalamu tunaozalisha hapa DMI na kwa maendeleo ambayo dunia imepitia hadi mwaka huu 2022 hatustahili kuendelea kuwa kwenye miundombinu chakavu kama hii,” amesema 

Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Dk. Tumaini Gurumo, amesema kusanyiko la wahitimu ni muhimu kwaajili ya kuwatambua wahitimu waliowahi kusoma kwenye chuo hicho sehemu walipo kwa sasa.

“Tunawakusanya na kuwasajili tunawaeleza chuo chao walichosoma kiko katika hali gani na tunawaeleza mipango yetu ya mbeleni na wao wanapata fursa ya kutoa maoni yao kuhusu kile walichokiona wakiwa wanasoma na hali ilivyo sasa na kushauri wapi tuelekee,” amesema Dk. Tumaini

Amesema kupitia kusanyiko hilo watajadili changamoto ya muda mrefu sana ya mafunzo ya vitendo kwa wahitimu wa chuo hicho ambayo huwa yanafanyika kwenye meli.

Dk. Tumaini ameishukuru serikali kwa kuendelea kuipa vifaa vya kufundishia na wahitimu kufanya mafunzo ya vitendo ambavyo hata hivyo bado havijakidhi mahitaji ya sasa ya wahitimu waliopo.

“Mtambo wa kufundisha wanafunzi kuendesha meli Stimulators ni muhimu kwa wahitimu kwani ndio unamwonyesha mhitimu kila kilichoko kwenye meli lakini pia mwisho wa siku lazima mhitimu aingie kwenye meli lakini inashindikana kwasababu hapa nchini hakuna meli za kutosha,” amesema

Aidha, amesema kama kungekuwa na meli nyingi za hapa nchini ingekuwa rahisi kuweka viwango kwa kila meli kuchukua kiasi cha wahitimu watano kwaajili ya mafunzo ya vitendo lakini fursa hiyo haipo.

“Tunategemea meli za nchi zingine zichukue wahitimu wetu kwaajili ya mafunzo ya vitendo huwa siyo rahisi sana kwasababu hizo meli zinakuwa nanafasi chache sana. Na ilimhitimu aive vizuri lazima apate mafunzo ya kwenye meli,” amesema

“Tunahitaji watu wa kutusemea huko kwenye vikao kwamba Tanzania imeingia makubaliano na baadhi ya nchi sasa yakitekelezwa vijana wetu watapata fursa nyingi za kufanya mafunzo ya vitendo,” amesema

Wakati huo huo chuo hicho kimepongezwa kwa kutoa Shahaza za Uzamili katika usafiri wa maji hali ambayo itasaidia kupata wataalamu wengi wa sekta ya usafiri wa majini.

Pongezi hizo zimetolewa leo na Meja Jenerali mstaafu, Said Shaaban ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) wakati akizunyumza kwenye kusanyiko hilo.

Amesema tangu kuanzishwa kwake chuo hicho kimefanikiwa kutoa wahitimu wengi wanaofanya kazi ndani na nje ya nchi katika sekta ya usafiri wa majini.

“Mahitaji ya wataalamu wa bahari bado ni makubwa sana hapa nchini ndiyo maana naona mchango wa DMI ni mkubwa sana katika kupata watu watakaofanyakazi kwenye usafiri wa majini ndani na nje ya nchi,” amesema