Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Mwanza
KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt.Jim Yonazi amesema hali ya lishe nchini imeendelea kuimarika kwa kuzingatia Takwimu zinaonesha kupungua kwa viwango vya utapiamlo kwa baadhi ya viashiria ikiwemo kiwango cha udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambacho ndio kiashiria kikuu cha utapiamlo kimepungua kutoka asilimia 32 mwaka 2018 hadi asilimia 30 mwaka 2022 (DHS 2022).
Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe nchini unaofanyika ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Malaika Jijini Mwanza,leo Oktoba 02,2024,uliowakutanisha wadau wa afua za lishe kwa lengo la kupokea na kujadili hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa afua za lishe kwa kipindi cha mwaka wa tatu 2023/2024 katika maeneo mahsusi yaliyoanishwa kwenye Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe (2021/22-2025/26).
Alieleza kuwa Mkutano huo unatoa fursa kwa wadau wote wa lishe kujadili namna utekelezaji ulivyofanyika, changamoto na mikakati ya kufanikisha utekelezaji katika kipindi kilichobaki cha utekelezaji wa mpango huo hususan mwaka 2025/26. Pia Mkutano huu unatazamiwa kuongeza msukumo mpya wa utekelezaji wa afua za lishe miongoni mwa wadau kama moja ya nguzo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Akiongelea kuhusu hali ya lishe amesema kuwa kiwango cha ukondefu pia kimepungua kutoka asilimia 3.8 mwaka 2014 hadi asilimia 3.5 mwaka 2018, ingawa takwimu hizi zilibadilika mwanzoni mwa mwaka 2023 baada ya kupata matokeo ya utafiti uliofanywa Machi – Julai 2022 na Taasisi ya Chakula na Lishe na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Dkt. Yonazi alisema kuwa, uwepo wa wadau katika mkutano huo ni uthibitisho tosha wa ushirikiano uliopo na utayari wao katika kuboresha hali ya lishe kwa Watanzania, hususan makundi yanayoathirika zaidi ambayo ni watoto wadogo na wachanga, watu wenye mahitaji maalum, wanawake wajawazito na wale walio katika umri wa uzazi.
“Naomba ushirikiano huo uendelee wakati wote wa utekelezaji wa mpango na hususan wakati kama huu ambao tunakutana kujadili utekelezaji Sote tunajua kuwa ili tuweze kuwa na maendeleo ya kiuchumi na kijamii ni lazima Taifa liwe na watu wenye lishe na afya bora ili kuwa na uwezo wa kufikiri, kutenda na kufanya kazi kwa bidii. Hivyo, juhudi hizi na nyingine ni muhimu kuwa endelevu ili kutuwezesha kufikia malengo,” alisisitiza Dkt. Yonazi.
Aidha Dkt. Yonazi alitumia mkutuno huu kuiasa jamii kuendelea kushiriki kikamilifu na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha hali ya lishe kwa Watanzania inaendelea kuimarika huku akisema kuwa Serikali inaahidi kuendelea kuunga mkono juhudi zilizopo na nyingine za wadau ili kuhakikisha Taifa linapata mafanikio dhidi ya mapambano ya tatizo la utapiamlo.
Kwa upande wake Mizengo Pinda Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema, Serikali imeendelea kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha jamii inaendelea na mapambano haya ya lishe duni na kuhakikisha Taifa linaendelea kuwa na watu wenye afya bora, na kukumbusha jamiii kuwa mstari wa mbele katika masuala ya afua za Lishe.
“Jambo hili la mapambano dhidi ya lishe ni Mtambuka, hakuna Wizara itakwepa, hivyo ni wakati sahihi na tuone njia sahihi za kutumia katika mapambano haya,ifike mahali tuizungumze dhana ya lishe katika wizara na kuhimiza agenda hii iwe ya kila mmoja,” alisema Mhe. Pinda
Aliongezea kuwa, masuala ya lishe yawekewe mkazo zaidi kuanzia katika elimu ya msingi hasa kupitia uwepo wa Klabu maalum zinazochagiza masuala ya afua za lishe nchini lengo ni kuwajengea uelewa watoto kuwa na elimu ya kina kuhusu masuala haya.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Anthony Mtaka alizungumza wakati wa mkutano huo alieleza jitihada zinazofanywa na mkoa wake katika mapambano dhidi ya Utapiamlo na masuala yote ya lishe amesema ni wakati sahihi kuwa na mikakati inayotekelezeka ili kuwa na jamii yenye lishe na afya bora.
Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe nchini umeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, na umebebwa na kauli mbiu isemayo “Kuchagiza Mchango wa Wadau wa Kisekta ili Kudumisha Matokeo Bora ya Hali ya Lishe Nchini Tanzania” ukilenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa pili wa Taifa wa Lishe ili kuendelea kukabiliana na changamoto za utapiamlo nchini.
More Stories
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto