November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Yonazi ateta na Maafisa habari

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online DODOMA

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amewataka Maafisa habari Serikalini kuendelea kuwa wabunifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Ametoa kauli hiyo Juni 20, 2023 Jijini Dodoma walipomtembelea katika Ofisi yake kwa lengo la kuangalia na kujifunza utendaji kazi wa vitengo vya Habari, Mawasilino na Uhusiano kwa Tanzania Bara.

Ugeni huo uliongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya habari Maelezo kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Idara ya Habari Maelezo Tanzania Bara pamoja na Maafisa mawasiliano kutoka katika Idara ya Habari Zanzibar, wa Wizara pamoja na Taasisi zilizopo Zanzibar.

Dkt. Yonazi alisema, ipo haja ya maafisa habari kubadili mitazamo katika kuhabarisha umma kwa kuangalia mabadiliko ya kiteknolojia kwa kutumia mifumo ya kisasa inayoendana na wakati uliopo.

“Endeleeni kuwa wabunifu katika kuibua habari na si kusubiri matukio ya viongozi ndipo mhabarishe umma, hakikisheni teknolojia haiwaachi nyuma bali mnaendana nayo katika kupashana habari,”alisema Dkt. Yonazi.

Aliongezea kuwa, pamoja na kuhabarisha ni muhimu kuandika habari zinazozingatia maadili na taaluma ili kuwa na habari zinazoshi na kuufaa umma.

Alitumia fursa hiyo kuwakumbusha maafisa habari kujali muda katika kutoa taarifa na vyanzo vya kuaminika ili kuepuka makosa yanayoweza kujitokeza endapo mambo hayo hayatazingatia.

“Lazima matukio na habari zitolewe kwa wakati na zenye ubora huku mkizingatia aina ya walaji wa habari hizo (audience) na kutumia njia sahihi za uwasilishaji wake,”alisisitiza Dkt. Yonazi

Sambamba na hilo aliwataka kuendelea kutoa habari za serikali kwa ufanisi huku akiwasisitiza kueleza mafanikio ya miradi ya kimkakati.

Aidha amewahimiza Maafisa habari kujifunza lugha zaidi ya moja ili kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu ya kuhabarisha umma kwani wanawafikiwa watu wengi ikiwemo wa mataifa mengine.