Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
ZIKIWA zimesalia siku mbili kuelekea Sikukuu ya Krismasi,jamii imetakiwa kuwa na moyo wa kujitolea kwa familia zinazoishi katika mazingira magumu, hususan zile zisizo na uwezo wa kupata chakula cha uhakika katika kipindi cha sikukuu, ili nazo zipate furaha badala ya kuishi katika hali ya unyonge.
Wito huo umetolewa Desemba 22, 2025 na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mbunge wa Jimbo la Uyole na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson, wakati akitoa msaada wa chakula na fedha kwa wahitaji katika Mtaa wa Mponja, Kata za Nsalaga Isyesye pamoja na Igawilo,kuelekea Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt.Tulia amesema zoezi hilo ni muendelezo wa msaada uliotolewa Desemba 21, 2025 ambapo walitembelea kata sita na kaya 54, huku Desemba 22 wakitembelea kata tano na kaya 48.

“Zoezi hili tutalihitimisha leo Desemba 23, 2025, na kwa kufanya hivyo tutakuwa tumefikia kata zote 13 za Jimbo la Uyole,” amesema.
Ameeleza kuwa wito wake kwa jamii ni kuendelea kusaidia wahitaji kwa sababu idadi yao ni kubwa zaidi ya wanaopata msaada kwa sasa.
“Hata kwa kidogo unachopata, toa ili kila mmoja aweze kuwa na furaha,” amesisitiza.
Dkt.Tulia ameongeza kuwa jamii inapaswa kujifunza kuwa na mioyo ya kutoa si kipindi cha sikukuu pekee, bali hata nyakati nyingine, kwa kuwa changamoto za maisha huwakumba watu muda wote.
“Jamii ikijenga utamaduni wa kusaidiana, huleta amani na mshikamano wa kweli,” amesema.
Kwa upande wake, Mratibu wa Tulia Trust katika Kata za Nsalaga na Igawilo, Lugano Mwangosi, amesema Dkt. Tulia ni kiongozi wa mfano anayestahili kuigwa, akifananisha mchango wake na maji ambayo mtu asipokunywa, basi huoga.
Mwangosi amesema kuwa baada ya zoezi la ugawaji wa chakula, mwezi Januari 2026 kutafanyika zoezi la ugawaji wa sare za shule kwa watoto 350 kutoka familia zenye uhitaji katika Kata ya Nsalaga.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Isyesye, Ambwene Mwakyusa, amemshukuru Dkt. Tulia kwa juhudi zake za kuendelea kusaidia watoto na familia zenye uhitaji.
Naye Diwani wa Kata ya Nsalaga, Clementi Mwandemba, amesema kata hiyo imejipanga kumuunga mkono kwa vitendo Mbunge wa Jimbo la Uyole ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa wananchi.
“Ndugu zangu wana Nsalaga, viongozi kama Dkt. Tulia hawapatikani kila mahali; hupatikana kwa mipango ya Mungu. Leo tumekusanyika hapa kwa tendo la huruma, ambapo Mbunge anaona na kugusa maisha ya watu wasio na uwezo, na kwa vitendo anatufundisha moyo wa kujitoa kwa wasiokuwa nacho,” amesema Mwandemba.


More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi