Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Uyole na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU),Dkt. Tulia Ackson, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa katika sekta ya elimu,hasa kuondoa changamoto zilizokuwa zikiwakabili wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika katika Kata ya Iduda, Septemba 29, 2025, Dkt.Tulia alisema awali wanafunzi walilazimika kusoma kwa awamu kutokana na uhaba wa madarasa na wengine walikaa chini kwa kukosa madawati, lakini changamoto hizo sasa zimepatiwa suluhisho.
“Ndugu zangu wa Iduda, tuna kila sababu ya kumchagua Rais Samia, mimi na Nchimbi. Katika sekta ya elimu tumefanya kazi kubwa. Hivi sasa hakuna mtoto anayekaa chini kwa kukosa dawati, na shule zetu zina vyumba vya madarasa vya kutosha,” alisema.

Ameongeza kuwa Shule ya Sekondari Iduda sasa imeboreshwa hadi kidato cha tano na sita, huku kukijengwa miundombinu ya maabara ili wanafunzi wapate elimu bora. Pia changamoto ya uchangishaji wa madawati kwa wazazi imekwisha.
Mbali na elimu, Dkt.Tulia amehaidi kumalizia ujenzi wa nyumba ya daktari katika Zahanati ya Iduda ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Amehimiza mshikamanano wa kisiasa, kuwataka wananchi wa Jimbo la Uyole na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025, kupiga kura na kuwachagua viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya urais, ubunge hadi udiwani.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma, Japason Lema, amesema Dkt. Tulia ni kiongozi anayepaswa kulindwa kutokana na mchango mkubwa anaoutoa katika maendeleo ya taifa.
“Dkt. Tulia ni mfano bora kwa vijana wanasiasa. Matendo yake ni darasa tosha kwa kila anayetaka kufika mbali kisiasa,” amesema Lema.
Aidha, Diwani wa Kata ya Iduda, Joseph Mwachemba, ameomba Dkt. Tulia kushughulikia changamoto ya barabara ya kiwango cha lami pamoja na uzio wa Shule ya Sekondari Iduda, ambayo sasa imekuwa kubwa na wanafunzi wake wanalala shuleni.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi