Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Uyole kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),Dkt.Tulia Ackson, ameahidi kuboresha shule zote za jimbo hilo, kuimarisha huduma za afya na kuendeleza jitihada za kuwawezesha wananchi kiuchumi iwapo atachaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Akihutubia wananchi wa Kata ya Ilemi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa James, Dkt.Tulia amesema atahakikisha shule za kata hiyo zinajengwa na kukarabatiwa madarasa mapya, huku akiboresha pia Kituo cha Afya Ilemi na Hospitali ya Igawilo.

“Nafahamu changamoto za shule zetu. Ni wajibu wangu kuhakikisha tunajenga na kukarabati madarasa ili mazingira ya watoto wetu yawe bora zaidi. Kama tulivyotekeleza barabara ya Mapelele, ndivyo pia nitakavyosimamia uboreshaji wa elimu katika jimbo hili,” amesema Dkt. Tulia.
Aidha,ameahidi kujenga barabara ya Juhudi kwa kiwango cha lami, akibainisha kuwa changamoto hiyo ya muda mrefu kwa wakazi wa Ilemi itapatiwa ufumbuzi.
“Tuliahidi barabara ya Mapelele mwaka 2020 na sasa imekamilika. Vilevile niliomba ridhaa kujenga barabara ya njia nne ambayo ujenzi wake unaendelea. Safari hii, barabara ya Juhudi na ile ya kuelekea Kituo cha Afya nitahakikisha zinajengwa mapema,” ameongeza.
Dkt.Tulia pia ameeleza kuwa serikali ya CCM imetekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ukiwemo ujenzi wa Shule ya Msingi Benson Mpesya, zahanati na kuboresha miundombinu mbalimbali katika jimbo hilo.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi (CCM) Tanzania Bara, Kilumbe Ng’enda, amewataka wananchi wa Uyole kumchagua Dkt.Tulia kwa mara nyingine, akisema historia yake ya maendeleo ni kielelezo cha uongozi bora.
“Ndugu zangu, tarehe 29 Oktoba msikosee. Chagueni mafiga matatu – Rais, Mbunge na Diwani ili tupate maendeleo zaidi. Kazi aliyofanya Dkt.Tulia mkiwa na ushahidi wa macho, sasa ni zamu yenu kumrudisha tena kwa kura zenu,” alisema Ng’enda.
Naye mgombea Udiwani wa Kata ya Ilemi kupitia CCM, Baraka Zambi, aliwataka wananchi kumlipa Dkt. Tulia kwa maendeleo aliyoyatekeleza.“Wananchi wa Ilemi tunalo deni kubwa kwake, Oktoba 29 tuonyeshe shukrani kwa kumpa kura ya ndiyo,” amesema Zambi.
Zambi pia amemuomba Dkt.Tulia kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami, kujenga vyumba vya madarasa na shule mpya ili kasi ya maendeleo iendelee kuonekana katika kata hiyo.


More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi