Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya
MBUNGE wa Jimbo la Mbeya Mjini na Spika wa Bunge Dkt.Tulia Ackson amefafanua kuwa taasisi ya Tulia Trust inawafikia na kuwajengea nyumba wahitaji na walio na maisha duni na si vingine.
Dkt.Tulia ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Tulia Trust amesema kuwa hakuna maombi yeyote ya kuomba kujengewa nyumba huku akieleza kuwa kuna baadhi ya watu wamekuwa wakipeleka maombi kwa taasisi hiyo wakiomba kusaidiwa kujengewa nyumba.
Hayo yamesemwa Aprili 10,mwaka huu wakati akimkabidhi nyumba Mama Mjane wa watoto sita aitwaye Singwava Jackson (50) mkazi mtaa wa Itanji Kata ya Iganjo jijini Mbeya ambaye kwa muda mrefu amekuwa akiishi kwenye kibanda kilichojengwa kwa miti na maturubai kabla ya Mbunge huyo kumjengea nyumba chini ya taasisi yake Tulia Trust .
“Sio kwamba wanaleta maombi ndugu zangu niseme wazi kabisa kuna watu wameanza kuleta maombi sisi hatufanyi kazi ya kuwajengea nyumba watu tunahitaji kuwasaidia wale walio kwenye dhiki na tunao uwezo wa kuwasaidia….., Mama Singwava yeye ni mmoja wao na hili jambo lilianza muda mrefu mchakato wake, ” amesema Dkt.Tulia .
Hata hivyo Dkt.Tulia amebainisha kuwa taasisi hiyo itaendelea kuwafikia watu wengi zaidi na kuomba Mungu kuwapa macho zaidi kuona wenye tabu zaidi ya wengine.
Aidha Dkt.Tulia amesema wataona wananchi wenye uhitaji na kwamba kuna watu wamekuwa wakidharau kila kinachofanywa kwa kudhani kuwa ni siasa.
“Lakini wanapiga maneno kama kule kwao hawajaona siasa zinazofanywa ,sasa niwaambie ndugu zangu wana Mbeya Mjini mimi sawa ni mwanasiasa hayo mambo ninayofanya kama yananisaidia kisiasa wacha yanisaidie lakini watu wanahudumiwa na wewe kama una uwezo wa kuhudumia fanya hujazuiwa ,kwa hivyo watanzania wenzangu tutaendelea kufanya kazi hii,”amesema Dkt.Tulia .
Akielezea zaidi Dkt.Tulia amesema wapo watu wenye mioyo menyepesi wanaposikia mambo kama hayo wanakata tamaa hivyo amewasii wenye moyo wa kusaidia wenye uhitaji wasaidie na wasikatishwe tamaa.
Akizungumza mbele ya Dkt. Tulia huku akitokwa machozi Mama mjane mwenye watoto sita ,Singwava Jackson (50)amesema kuwa aliolewa Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe ambapo baada ya mume wake kufariki ndugu wa mume walimfukuza na kuamua kuja jijini Mbeya kuanza maisha kwa kuokota makopo na kuuza kwa sh.150 kwa kila kopo.
Kutokana na biashara hiyo alifanikiwa kununua kiwanja kwa milioni.1 Kata ya Iganjo na kufanikiwa kujenga na kuezeka kwa kutumia maturubai kuanzia chini mpaka juu.
Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC)kutoka Mkoa wa Mbeya Ndele Mwaselela amewataka viongozi kuanzia shina kutengeneza mkakati wa kulinda heshima ya Dkt.Tulia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na kutodiriki kuleta rangi mbili ambayo ni tofauti na kwamba kabla ya kwenda sehemu nyingine wasafishe nyumba yao kwanza kwa maana wao wapo wengi.
Hata hivyo Mwaselela ametoa agizo kwa Katibu Mwenezi na Itikadi wa CCM kuhakikisha kuwa popote watakaposimama waseme kazi nzuri zinazofanywa na Dkt.Tulia pamoja na kumlinda na kusema watu wenye wivu siku zote huwa hawapendi maendeleo.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi