Na Esther Macha, Timesmajira, Online Mbeya
SPIKA wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Dkt. Tulia Ackson, ameahidi kuungana na Halmashauri ya Jiji la Mbeya katika kuwezesha wanafunzi wa kike taulo kwa ajili ya kutumia wakati wa hedhi.
Huku akiitaka Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuongeza jitihada za kuwawezesha wanafunzi wa kike katika Jiji hilo ili waweze kupata elimu katika mazingira rafiki hasa wakati wa siku zao za hedhi.
Dkt. Tulia ameyasema hayo leo wakati wa hafla ya kukabidhi taulo za kike 4000 kupitia mfuko wa Halmashauri zenye thamani ya milioni 10 kwa Wakuu wa Shule za Sekondari na Msingi za Serikali iliyofanyika katika shule ya sekondari ya wasichana Loleza.
Pamoja na kuishukuru Halmashauri kwa msaada huo, amesisitiza kuwa bado idadi inayotolewa ni ndogo kulingana na uhitaji wake na ameahidi kushirikiana nao ili kuhakikisha taulo nyingi zaidi zinazopatikana kukidhi mahitaji.
“Nitahakikisha naungana nanyi katika utoaji wa taulo hizi za kike kwani bado idadi ndogo ukilinganisha na mahitaji ya watoto wetu wa kike,”amesema Dkt.Tulia.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya Dormohamed Issa, amemshukuru na kumpongeza Dkt. Tulia kwa jitihada ambazo amekuwa akizifanya katika Jiji hilo ikiwemo kuwaunganisha wananchi na serikali yao na kuwezesha kupata mafanikio ya haraka kila kukicha.
Amesema kuwa watahakikisha wanashirikiana kwa pamoja lengo likiwa kuleta maendeleo ya pamoja na kutatua changamoto za wananchi.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba