Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya
SPIKA wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Dkt.Tulia Ackson amewatolea uvivu baadhi ya watu wanaomuandama mitandaoni kuwa anawatangaza watu anaowapa misaada, akieleza kuwa anafanya hivyo ili kutoa funzo kwa wengine kuiga mfano wa kuwasaidia wahitaji.
Dkt.Tulia ametoa kauli hiyo Januari 22,2024 wakati alipoiongoza taasisi ya Tulia Trust kutoa msaada wa sare za shule na madaftari kwa wanafunzi 3000 wa shule za msingi wanaoishi kwenye mazingira magumu jijini Mbeya.
Dk.Tulia amesema wapo baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii ambao wanamshukia kuwa hapaswi kuwatangaza watu ambao wanapewa misaada na taasisi yake au yeye binafsi.
Amesema anafanya hivyo ili kutoa funzo kwa wengine kutambua wajibu wao wa kuwasaidia watu wanaoishi kwenye mazingira magumu, akitoa wito Kwa jamii kuwa na utamaduni wa kujitolea Kwa watoto ambao wanapitia changamoto za maisha kutokana na hali duni za maisha.
“Mahitaji haya ambayo ni sare na madaftari yanawahusu wanafunzi wa darasa kwanza hadi la nne wanaotoka kwenye familia zenye changamoto,sisi pia tuna hilo jukumu ya kusaidia wengine anza na jirani yako asilale njaa, usisubiri uwe na kikubwa hicho hicho ulicho nacho kinatosha,”amesema.
Amesema serikali kwa kiwango kikubwa imeboresha miundombinu ya elimu katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya ikiwemo kujenga matundu ya vyoo zaidi ya 310.
Hata hivyo amesema kazi ya kuboresha sekta ya elimu ni endelevu na inagusia maeneo mengi ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na shule kwenye maeneo ambayo hayana huduma ya elimu.
Kwa upande wake Ofisa Elimu Msingi Jiji la Mbeya, Julius Lwinga amesema Halmashauri ina jumla ya wanafunzi 103,400 na walimu 2252 ambao wanatosheleza mahitaji ya wanafunzi.
Amesema pia Jiji hilo lina shule za msingi 105 ambapo kati ya hizo 83 ni za serikali na 22 ni zile zinazomilikiwa na taasisi za Dini na watu binafsi.
Amesema wanafunzi walengwa 3000 ambao wamepatiwa msaada wa sare na madaftari wamepatikana baada ya kufanyika mchakato uliozingatia vigezo vya hali ya changamoto ya kimaisha kutoka kwenye familia zao.
“Mwaka 2023 halmashauri yetu ilikuwa ya tano kitaifa kwa ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba baada ya kupata asilimia 97.3,”amesema.
More Stories
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo