Na Esther Macha,TimesMajiraOnline,Mbeya
MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Uyole kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM),Dkt. Tulia Ackson, ameahidi kuhakikisha wananchi wa Kata ya Mwakibete ambao bado hawajafikiwa na Mradi wa Umeme Vijijini (REA) wanapata huduma hiyo, ili kuondokana na changamoto ya kukosa nishati hiyo muhimu.
Dkt.Tulia ametoa ahadi hiyo Oktoba 3, 2025, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la Magereza,Mtaa wa Viwandani,Kata ya Mwakibete.Amesema kuwa kwa sasa asilimia kubwa ya wananchi wa Jimbo la Uyole tayari wameunganishwa na umeme kupitia REA na kuahidi kufuatilia kwa karibu ili kuhakikisha walioachwa nyuma nao wananufaika.
“Sisi Uyole ni kazi na tukisema tunatekeleza kwa vitendo.Nitahakikisha wananchi wote wanapata huduma ya umeme wa REA kama ambavyo wenzao tayari wamenufaika,”amesema Dkt.Tulia.
Aidha,amempongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa hatua kubwa ya kuondoa mgao wa umeme nchini baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, linalozalisha umeme wa uhakika kwa Watanzania.
“Ndugu zangu, leo hakuna mgao wa umeme. Rais Samia amehakikisha fedha zinapatikana na sasa tunazalisha umeme mwingi, kiasi cha kuweza kuuza hata nchi nyingine. Changamoto kubwa ya nishati imepatiwa suluhisho,”ameongeza Dkt. Tulia.

Akizungumzia zaidi,amesema kuwa mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere utabaki kuwa nguzo ya maendeleo kwa Watanzania kutokana na uzalishaji mkubwa wa umeme.
Amesisitiza kuwa wapiga kura wa Mwakibete wana wajibu wa kumpa heshima Rais Samia kupitia kura zao ili miradi ya nishati, hususan umeme wa REA,iendelee kusogea mbele.
Kwa upande wake, Mgombea udiwani wa Kata ya Mwakibete kupitia CCM, Lucas Mwampiki, amemshukuru Dkt. Tulia kwa jitihada zake za kusukuma miradi ya maendeleo katika kata hiyo. Alisema wakazi wa Mwakibete wana deni kubwa la kuendelea kumuunga mkono Rais Samia na Mbunge wao Dkt. Tulia kutokana na utekelezaji wa miradi mingi ikiwamo:
Ujenzi wa daraja linalounganisha Kata za Mwakibete, Tembela na Mwasanga, ambalo sasa limekuwa kivutio.
Ujenzi wa Kituo cha Afya na kupeleka gari la wagonjwa.
Ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari Mwakibete na Shule ya Msingi Bombambili.
Upatikanaji wa madawati ya kutosha kwa shule zote za sekondari na msingi katika kata hiyo.
Mwampiki amesisitiza kuwa utekelezaji huo wa miradi ni ishara tosha ya dhamira ya serikali ya CCM kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi