Na,Esther Macha, Timesmajira, Online,Mbeya
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Tulia Ackson ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya mjini amewataka Wananchi kupuuza taarifa zinazosambazwa na baadhi ya watu kuhusiana na mkataba wa Bandari.
Spika Dkt. Tulia amesema hayo leo,Juali 13,2023 katika ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo katika kata mbalimbali za Jiji la Mbeya ambapo amesema Watanzania wasiwe na wasiwasi Nchi ipo salama chini ya Rais Dkt Samia Suluhu.
Amesema wapo watu wamekua wakisambaza taarifa za upotoshaji kwa Wananchi kuhusiana na suala la Bandari wakidai Serikali imeingia mkataba wa muda mrefu jambo ambalo sio la kweli.
Ameeleza kilichofanyika ni Serikali kuingia makubaliano ya ushirikiano wa uendeshaji wa Bandari na sio mkataba kama inavyoolezwa na kusambazwa na baadhi ya watu.
“Kuna watu kazi yao ni kupinga kila kitu na kusambaza habari za uongo, mimi mtoto wenu mmenisomesha tena nimekuwa daktari wa sheria hakuna kitu kitakachoharibika, Nchi iko salama na itakua salama na Rais Samia ana nia nzuri na Watanzania” amesema Dkt. Tulia.
Ameongeza kuwa taarifa hizo zinapaswa kupuuzwa kwa kuwa wapotoshaji hao hawana uhakika na jambo wanalolisema na kwamba kazi yao kubwa ni kupotosha kila jambo linalofanywa na serikali.
Katika Ziara hiyo Dkt. Tulia ametembelea Shule ya Msingi Iwambi ambapo ametoa msaada wa mifuko 100 ya saruji na fedha taslimu shilingi milioni mbili kwa ajili ya kusaidia ukarabati wa miundombinu ya madarasa.
Mbali na shule hiyo pia Dkt.Tulia ametoa msaada katika Shule ya Sekondari Maziwa iliyopo katika Kata ya Iyunga, Shule ya Sekondari Dk. Tulia iliyopo kata ya Itende na kuweka Jiwe la Msingi ujenzi wa Ofisi ya afisa mtendaji Kata ya Ruanda.
Awali mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Dor Mohammed ametoa wito kwa wakazi wa Jiji la Mbeya kumuunga mkono Dk. Tulia kwa juhudi zake za kuwaletea maendeleo.
Amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya Ubunge wa Dkt. Tulia Jiji la Mbeya limepokea zaidi ya shilingi bilioni 15 katika sekta ya afya na elimu pekee jambo ambalo wabunge waliotangulia hawakufanya.
Aidha amesema maendeleo ya Jiji la Mbeya yamekuwa yakiongezeka kwa kasi sana kutokana na uwepo wa Dkt. Tulia kwa sababu ya usikivu na unyenyekevu alionao pamoja na maelewano yake na Rais Samia hivyo jambo lolote akiomba anakubaliwa.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato