March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Tulia atoa wito kwa jamii kujenga desturi kusaidia wasiojiweza

Na Esther Macha,TimesMajira Online,Mbeya

JAMII imetakiwa kujenga utamaduni wa kusaidiana, hususan kuwasaidia watu binafsi wanapokumbwa na changamoto mbalimbali za kimaisha, ikiwemo majanga ya kuungua kwa nyumba na kupoteza mali muhimu, ili kuimarisha mshikamano na usawa katika jamii.

Wito huo umetolewa na Spika Mstaafu wa Bunge la Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Uyole, alipotoa msaada wa mabati bando tano kwa familia moja iliyokumbwa na mkasa wa kuungua kwa nyumba, ambapo walishindwa kuokoa mali zao.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Dkt.Tulia amesema jamii ina wajibu wa kujenga desturi ya kusaidiana, hasa pale mtu au familia inapokumbwa na changamoto kubwa.

“Kama jamii tujenge desturi ya kusaidia mtu mmoja mmoja anapopata changamoto katika maeneo yao. Huu uwe utamaduni wetu. Tukisaidiana kwa namna hii, familia hizi zitapata faraja kupitia sisi wananchi,” amesema Dkt Tulia.

Kwa upande wake, Esther Kyanula, mama wa familia iliyokumbwa na tukio hilo, alimshukuru Dkt Tulia kwa msaada alioutoa, akisema umeirejeshea familia yao matumaini mapya.

“Dkt Tulia ametupa tumaini jipya. Familia yetu imefarijika sana na tunaendelea kumuombea. Tunafahamu amekuwa akigusa maisha ya familia nyingi zinazoishi katika mazingira magumu, ikiwemo zile zisizo na makazi,” amesema.

Wananchi wengine, Elinetha Fumbo na Michael Kapungu, nao walimshukuru Dkt Tulia na kumuomba aendelee kushirikiana na jamii katika nyakati za shida na raha.

Naye Mratibu wa Taasisi ya Tulia Trust katika Kata ya Igawilo, Lugano Mwangosi, aliwashukuru wananchi kwa ushirikiano waliouonyesha katika kusaidia familia hiyo.

Taasisi ya Tulia Trust, chini ya Mkurugenzi wake Dkt Tulia Ackson, imekuwa ikiendelea kutoa misaada mbalimbali kwa makundi yenye uhitaji katika maeneo tofauti nchini, ikiwemo kujenga nyumba zaidi ya 22 ndani na nje ya Mkoa wa Mbeya, kusomesha watoto wanaotoka katika familia duni, pamoja na kutoa misaada ya vyakula na mahitaji mengine muhimu.