Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya
MBUNGE wa Jimbo la Mbeya Mjini na Spika wa Bunge ambaye ni Rais Umoja wa Mabunge Duniani,Dkt.Tulia Ackson amekabidhi msaada wa mahitaji mbalimbali kwa waathirika ambao nyumba zao zilifunikwa na maporomoko ya tope katika Mlimani Kawetele Kata ya Itezi jijini hapa na kusababisha kukosa makazi ya kuishi.
Ambayo yaliotokea Aprili 14, 2024 na kusababisha nyumba 20 na shule kufunikwa na maporomoko ya tope huku wananchi wakikosa makazi ya kuishi ambao kwa sasa wamehifadhiwa katika shule ya msingi Tambulikareli ambayo imefungwa kwa muda wakati utaratibu mwingine wa kuwahifadhi wananchi hao na familia zao ukiendelea.
Msaada huo umekabidhiwa Aprili 16, 2024 na Katibu wa Mbunge Jimbo la Mbeya Mjini,Steven Chambanenge kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo hilo Dkt.Tulia .
Vitu vilivyokabidhiwa ni pamoja na kilo 200 za mchele,unga wa ugali kilo 500, maharage kilo 80,majiko 20 ya gesi ,sukari kilo 200,lita 50 za mafuta ya kupikia ili viweze kuwasaidia waathirika wa maporomoko hayo.
Dkt. Tulia ambae kwasasa yupo nchini Marekani kushiriki kikao cha kujadili changamoto za mabadiliko ya tabia nchi yanayoikumba Dunia na utatuzi wake, wakati wa mkutano wa mwaka 2024 wa Jukwaa la Kibunge la Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani.
Mkutano huo ulioanza Aprili 15 ,2024 katika makao makuu ya Benki ya Dunia, Washington DC, nchini Marekani.
Diwani wa Kata ya Itezi Sambwee Shitambala ameshukuru kufuatia msaada huo uliotolewa na Mbunge huyo huku akiomba wadau wengine kujitokeza kusaidia wananchi waliopatwa na janga hilo na kusema uhitaji bado mkubwa.
Pia Shitambala amesema bado kuna changamoto ya vyoo kuwa vichache, uhaba wa maji na umeme huku akipongeza mwitikio wa wadau zikiwemo taasisi za serikali,binafsi na watu binafsi.
Mratibu wa maafa Mkoa wa Mbeya,Juma Maduhu amesema mahitaji ya sasa kwa waathirika hao ni zaidi ya tani saba za chakula ikiwemo mchele, unga na nafaka nyinginezo ambazo ni kwa ajili ya mboga.
Huku akieleza kuwa kama kitengo cha maafa walichukua hatua za awali ikiwa ni kutoa msaada wa vifaa mbalimbali ikiwemo mablangeti,magodoro na ndoo.
“Bado tunaendelea kuhamasisha wadau kujitokeza kusaidia wananchi hawa kwani bado uhitaji ni mkubwa,”amesema.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu