March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Tulia amnadi Rais Samia,ataja matokeo chanya ndani ya siku 100

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

SPIKA wa Bunge na Mgombea Ubunge wa Jimbo jipya la Uyole kupitia CCM, Dkt.Tulia Ackson,amesema kuwa katika siku 100 za uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, Watanzania wataona matokeo chanya hususan kwa vijana.

Amesema Rais Samia ameahidi kwamba akishinda kwa kura za heshima,ataongeza fedha kwa ajili ya vijana,kwa kuwa asilimia 10 zinazotolewa na halmashauri hazitoshelezi mahitaji yaliyopo.

Akizungumza Septemba 23, 2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Mwasanga,Mtaa wa Nsoho,Dkt.Tulia amesema kuwa siku 100 za rahisi Samia zitakuwa za mafanikio makubwa na Neema.

“Rais amesema anajua fedha zinazotolewa na halmashauri ni ndogo,ndiyo maana ameahidi kuongeza ili shughuli za vijana na uchumi wetu usonge mbele.”

Aidha,Dkt.Tulia alieleza kuwa katika Ilani ya CCM 2025–2030, serikali imejipanga kuendelea kutoa ruzuku ya pembejeo za kilimo na kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja.

“Serikali inalipia gharama kubwa ili pembejeo ziweze kuuzwa kwa bei nafuu, jambo litakalosaidia wananchi kupiga hatua na kuondokana na umasikini,” amesema.

Kwa upande wake,Diwani Mteule wa CCM, Brandy Nelson,ameomba msaada wa barabara na shule ya msingi kutokana na changamoto kubwa inayowakabili wakazi wa kata hiyo.
“Mama yetu, tunaomba tusaidiwe barabara na shule, hali ni ngumu. Najua mambo yako ni ya haraka, hivyo wananchi wakijitokeza kupiga kura maendeleo yetu yataimarika zaidi,” alisema Brandy huku akipiga magoti akiomba msaada huo.

Suma Fyandomo,Mbunge Mteule kupitia Umoja wa Wanawake,naye aliwataka wakazi wa Uyole kumpa kura Rais Samia pamoja na wagombea wengine wa CCM ili miradi ya maendeleo iendelee kusonga mbele.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Mkoa wa Mbeya, Edina Mwaigomele, amesema takwimu zinaonyesha wanawake wengi wanashiriki katika shughuli za maendeleo na hivyo kumuhitaji Rais Samia aendelee kuwa mstari wa mbele katika kuwawezesha.