December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Tulia awataka wanahabari kuokoa rasilimali pwani

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

SPIKA wa Bunge ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani(IPU)Dkt.Tulia Ackson amesema watu milioni 16 nchini wanategemea rasilimali za Pwani hivyo ametoa rai kwa waandishi wa habari kutumia karamu zao kuokoa rasilimali hizo hasa kwa kutoa elimu kwani uharibifu wa mazingira haufanyiki Tanzania Bara pekee bali hata ukanda wa Pwani.

Dkt.Tulia amesema hayo jijini hapa leo,Mei 2,2024
kwenye uzinduzi wa  Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani wakati akizungumza na Waandishi wa Habari,Wadau wa Habari wakiwemo Viongozi wa Serikali na Asasi za kiraia.

Ambapi amewataka Waandishi wa Habari nchini kuielimisha Jamii kuhusiana na mabadiliko ya Tabianchi kutokana na kuwepo kwa athari mbalimbali zilizotokana na mafuriko.

Vilevile amewataka Waandishi wa Habari kuhakikisha wanazingatia suala la usawa  wa kijinsia katika kuripoti Habari za uchaguzi ili kutenda haki kwa Wagombea.

“Mzingatie suala la kijinsi kwa watu wote siyo tu kwa wanawake lakini hata kwa wanaume pia ili kutenda haki hasa katika suala lilipo mbele yetu la uchaguzi wa Serikalini za mitaa,”amesema Dkt.Tulia

Kwa upande Wake Waziri wa Habari,Mawasiliano na teknolojia ya Habari Nape Nnauye amewataka wanahabari kuhamasisha watanzania  kugombea nafasi mbalimbali za Uongozi huku akiwataka Waandishi wa Habari kutenda haki wakati  wa kuripoti taarifa za wagombea bila kujali vyama vyao. 

Aidha Waziri Nape amelishukuru Bunge kwa mapendekezo ya Sheria ya Habari huku akisema kuwa Changamoto kubwa iliyopo  ni uchumi wa vyombo vya habari hivyo Kama Serikali wataliangalia suala hilo  kwa Kulipa madeni ili viweze  kuimarika.

“Yapo mambo mengi yamefanyika kuzingatia uhuru wa Vyombo vya Habari hivyo kuna mabadiliko ili kuhakikisha uhuru wa habari unaimarika,Uhuru  wa Vyombo vya habari sio tu uhuru wa Demokrasia bali ni demokrasia yenyewe,”amesema.

Awali Rais wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC)Deogratius Nsokolo,amesema kuwa Waandishi ni Afya  ya ustawi wa jamii  na ni chachu katika maendeleo hivyo wana imani na serikali kuendelea kulisikiliza kundi la wanahabari nakuzifanyia kazi changamoto ambazo zimekuwa zikiwakwaza  kwenye  kazi ya Habari.