Na Joyce Kasiki, Kilombero
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Dkt. Stergomena Tax kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kuongoza Wizara hiyo ,ametembelea mradi wa skimu ya umwagiliaji iliyojengwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambao umelenga kuzalisha zao la mpunga mara mbili kwa mwaka.
Mradi huo unatekelezwa na JKT katika kikosi cha jeshi hilo cha 837 KJ, Chita JKT katika kijiji cha Chita wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro .
Akizungumza mara baada ya kutembelea mradi huo Dkt.Tax amelipongeza JKT kwa kuanzisha mradi huo huku akisema unakwemda kuisaidia Serikali katika usalama na upatikanaji wa chakula.
Ametumia nafasi hiyo kuliagiza Jeshi hilo kuwa wabunifu katika kutafuta raslimali fedha ili kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya skimu hiyo ili kuongeza uzalishaji zaidi ambao utalifanya Jeshi hilo liweze kujitosheleza kwa Chakula.
“Mjitahidi kutafuta rasilimalifedha ili kukamilisha ujenzi wa skimu hii lakini na mimi nitashirikiana nanyi katika kutafuta fedha hizo ” alisema dkt. Tax
Pia aliishukuru Serikali kwa kulipatia Jeshi hilo Sh3.5 bilioni, fedha zitakazosaidia kuongeza vitendea kazi ikiwemo matrekta na vifaa vya kuvuna.
Waziri Tax amezungumzia kuhusu mbegu ambapo amesema ,mbegu imekuwa ni tatizo kubwa sana duniani na hivyo hatua iliyochukuliwa ya JKT ya kuzalisha mbegu ya mpunga katika kikosi hicho ni ya kujivunia na kupongezwa.
“Kama mtu ana miradi mikubwa ya kilimo halafu haba mbegu inakuwa ni kazi bure kwa sababu atakuwa hana cha kupanda ingawa amelima mashamba makubwa,lakini kwa uzalishaji huu wa mbegu mnajihakikishia upatikanaji wa mbegu bora ambazo zitakwenda kutoa mazao bora”amesisitiza
Kwa upande wa vijana wanaojiunga na JKT, Dkt Tax aliwataka vijana wanaopata fursa ya kujiunga na JKT kutumia nafasi hiyo vizuri kwa sababu sio kila mtu anapata fursa ya kujifunza na kutumia mitambo ya kisasa ya kilimo, ufugaji na uvuvi.
Pia amelitaka jeshi hilo kuhakikisha kuwa linazalisha zaidi chakula hasa ukizingatia Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA) imeshatangaza juu ya kuwepo upungufu wa mvua unaoweza kusababisha upungufu wa chakula nchini.
Kuhusu miaka 60 ya uhuru, Dkt. Tax alisema jeshi lina jukumu la kuwajenga vijana kiuzalendo ili waweze kuwa vijana waliokamilika, ulinzi na uzalishaji.
Amesema miradi inayofanyika ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika kikosi hicho cha mafanikio JKT yaliyopatikana ndani ya miaka 60 tangu uhuru Tanzania Bara
“Mradi wa mwagiliaji ni mkubwa inaweza kwa kiasi kikubwa kulisha vijana wetu wa JKT. Kama mnavyofahamu usalama wa chakula ni kitu muhumu katika usalama,”amesema. Kuhusu ufugaji wa samaki amesema mabwawa ya samaki yameanza ufugaji wa kitoweo , na kwamba lengo la kuzalisha tani 12 litafikiwa kwa haraka sana na hivyo kulisha nchi na hadi nje ya nchi.
Naye Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele amesema miundombinu inayojengwa katika kikosi hicho inahitaji fedha nyingi.
Amesema hadi sasa mifumo ya umwagiliaji katika mashamba hayo imekamilika kwa asilimia 50 kwa kutumia fedha za kutoka vyanzo vyao vya ndani ikiwemo Suma JKT.
Vilevile amesema miundombinu hiyo imefanya kutumia takribani Sh4 bilioni na hivyo ili kukamilisha miradi hiyo inahitaji kiasi kisichopungua Shilingi bilioni 8.
Amesema wameanza kutumia maji ya kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kwa kuingiza maji katika sehemu ya mashamba ya mbegu.
Kwa mujibu wa Meja Jenerali Mabele lengo kulima mara mbili kwa mwaka masika na kiangazi na kwamba wakati wa kiangazi mazao yatakayopatikana yatakuwa mengi.
Amesema mazao yatakuwa mengi wakati wa kiangazi kwasababu watatumia maji kuingiza shambani kwa kiasi kinachotakiwa na kuyatoa yanapozidi na hivyo mbolea itakaa shambani tofauti na masika ambapo unaweza ukaweka mbolea ikaja mvua nyingi inaiondoa.
More Stories
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili