
NNa Joyce Kasiki,Timesmajira
KATIKA jitihada za kulinda afya ya jamii na mazingira, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeendelea kuwa chombo muhimu na cha kipekee nchini kinachotekeleza majukumu ya kisayansi kwa umahiri na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.
Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira wa mamlaka hiyo Dkt. Peter Shimo , alipokuwa akizungumza kwenye Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) jijini Dar es Salaam.
Historia na Majukumu
Dkt. Shimo alieleza kuwa mamlaka hiyo ilianza rasmi mnamo mwaka 1995, ingawa historia yake inaanzia enzi za ukoloni. Kwa sasa, Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali inahusika na uchunguzi wa sampuli mbalimbali kutoka kwenye mazingira yetu ya kila siku, zikiwemo sampuli zinazotokana na majanga, sumu, uchafuzi wa mazingira, tiba na hata sampuli zinazohusiana na uhalifu wa kijinai.
“Katika huduma za afya, tunafanya uchunguzi wa vinasaba ili kuthibitisha uhusiano wa kimwili, kama vile kati ya mtoaji na mpokeaji figo, au kwa watoto wanaozaliwa na jinsia mbili ili kubaini utawala wa kijinsia kwa ajili ya matibabu sahihi,” alisema Dkt. Shimwe.
Udhibiti wa Matumizi ya Kemikali
Alisema,Mamlaka hiyo pia ndiyo msimamizi wa utekelezaji wa Sheria ya Kudhibiti Matumizi ya Kemikali ya mwaka 2003, ambapo mtu yeyote anayehusika na kemikali iwe ni kuingiza, kusafirisha, kutumia au kuhifadhi anapaswa kusajiliwa na Mkemia Mkuu wa Serikali, kama msajili wa kisheria.
Kupitia huduma hiyo mamlaka imewezesha usalama wa afya kwa wananchi na mazingira kwa ujumla, huku ikihakikisha kwamba shughuli zote za kemikali nchini zinazingatia viwango na taratibu sahihi za kisheria na kisayansi.
Kituo cha Taifa cha kuratibu Matukio ya sumu
Katika kuhakikisha usalama wa afya ya Umma alisema, Mamlaka inaendesha Kituo cha Taifa cha Kuratibu Matukio ya Sumu, kinachosimamiwa moja kwa moja na Mkemia Mkuu wa Serikali. Kituo hiki kinasaidia katika kutoa matokeo kwa haraka ili wagonjwa wapate matibabu stahiki kwa wakati, hasa katika matukio ya dharura yanayohusisha sumu.
“Matokeo ya kazi zetu si tu yanawezesha matibabu, bali pia yanasaidia katika usimamizi wa haki, kutambua uhalifu na kuthibitisha ushahidi wa kisayansi mahakamani,” aliongeza Dkt. Shimo.
Elimu na Ushirikiano na Wananchi
Katika maonyesho ya Sabasaba, Mamlaka inahamasisha wananchi kutembelea banda lake ili kufahamu kwa undani shughuli mbalimbali zinazofanywa, huku wito ukiwa kwa wanafunzi wa mchepuo wa sayansi kuwatembelea wataalamu wa taasisi hiyo kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo.
“Hii ni taasisi ya kisayansi. Wanafunzi wanaopenda masomo ya sayansi wana nafasi kubwa ya kunufaika kwa kujifunza mbinu mbalimbali za uchunguzi wa kisayansi,” alisema Dkt. Shimo.
Aidha, wajasiriamali wanaojihusisha na kemikali wanashauriwa kufika ili kujisajili kwa njia ya kidijitali na kupata ushauri kuhusu namna salama na sahihi ya kutumia kemikali kisheria.
Ubora na Uthibitisho wa Matokeo
Alisema huduma zinazotolewa na mamlaka hii zimepitia mchakato wa ithibati na zinatambulika kisheria kwa viwango vya kitaifa na kimataifa. Hii imejenga imani kubwa kwa wananchi, hasa kutokana na ukweli kwamba matokeo yanayotolewa ni sahihi, yenye uthibitisho wa kisayansi na yanayoweza kutumika kwenye vyombo vya sheria na tiba.
“Kwa ujumla, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ni nguzo muhimu katika kulinda afya ya jamii, kusimamia mazingira salama, kudhibiti kemikali na kusaidia haki kutendeka. Kupitia ushiriki wake katika maonyesho ya Sabasaba, mamlaka hiyo inalenga kutoa elimu kwa wananchi na kuwahamasisha kushirikiana katika kulinda usalama wa kiafya na kimazingira kwa maendeleo ya Taifa.
“Tunawakaribisha wananchi wote kutembelea banda letu. Hii ni nafasi ya pekee kwa kila mmoja kujifunza na kuelewa namna sayansi inavyoweza kuleta suluhisho katika maisha ya kila siku,” alihitimisha Dkt. Shimo

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi