December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt Seseja:Lengo la ukusanyaji chupa za damu zinazokidhi mahitaji ya nchi nzima bado halijafikiwa

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

KAIMU Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Dkt.Samwel Seseja amesema pamoja na jitihada za uhamasishaji wa kuchangia damu nchini Tanzania,Mpango wa Taifa wa Damu Salama bado haujaweza kufikia lengo la kukusanya chupa za damu  zinazokidhi mahitaji ya nchi nzima.

Amesema mahitaji ya damu kwa mwaka 2022 ni chupa 550,000 ambayo ni asilimia 1 ya idadi ya wananchi kwa makadirio ya takwimu za mwaka 2020 huku malengo ya mwaka 2022 ni kukusanya chupa 375,000 ambazo ni asilimia 70 ya mahitaji yote.

Dkt.Sseseja amesema hayo jijini hapa leo  ikiwa ni wiki ya  kampeni ya siku ya achangiaji damu duniani,ambayo huanza kuazimishwa  1-14/06 kila mwaka kwa dhumuni la kuongeza ufahamu wa hitaji la damu salama na bidhaa za damu kwa ajili ya wahitaji wa damu.

“Mpango wa Taifa wa Damu Salama kwa kipindi cha mwaka 2020/2021 kwa kushirikiana na timu za halmashauri wameweza kukusanya chupa za damu 331,279 ambayo ni sawa na asilimia 88 ya lengo na asilimia 60 ya mahitaji ya nchi,”amesema.

Amesema ,kwa kutumia vigezo vya  shirika la afya duniani (WHO)Nchi inahitajika kukusanya damu asilimia 1 ya wakazi wake au chupa 10 kwa kila wananchi 1000 na kwamba kwa Tanzania Hadi sasa zimefikia chupa 6 kwa kila watu 1000.

Hata hivyo Dkt.Seseja ameleza kuwa malengo ya makusanyo katika Maadhimisho ya siku ya Mchangia Damu Duniani kwa mwaka huu ni kwamba timu zote za ukusanyaji damu nchini ngazi ya Kanda, Hospitali ya Taifa, Hospitali za Rufaa, Mikoa na Halmashauri zimeshiriki kampeni ya ukusanyaji damu lengo likiwa kukusanya jumla ya chupa 45,532 kwa mgawanyo wa angalau kila kituo kukusanya asilimia saba (7%) ya malengo yake yaliyowekwa kutokana na idadi ya watu.

Ameeleza kuwa  uchangiaji wa damu wa hiari wa kujirudia unahitajika ili kuhakikisha damu inapatikana kwa wanaotakiwa kuongezewa damu mara dharura zinapojitokeza.

“Kama mwananchi unaweza kusaidia uwepo wa damu katika hospitali zetu na kwa muda wote kwa kuchukua kuchangia damu katika kampeni hii na kwa kufanya hivyo utasaidia kuokoa maisha ya mgonjwa mwenye uhitaji wa damu katika jamii,”amesema.

Kwa upande wake Meneja wa Damu salama kanda ya kati Dkt.Katura Mathius,ameeleza vigezo vya mchangia damu kuwa kabla ya kuchangia damu unapaswa kupima uzito wa mwili,kupima wingi wa damu(Hb),kupima mgandamizo wa damu(Blood Pressure),kupima mapigo ya moyo na ushauri nasaha na kwamba baada ya kuchangia damu vipimo hufanyika maabara za kanda ili kubaini kundi la damu.

Huku akitaja wahitaji wa damu nchini kuwa ni pamoja na watoto chini ya Umri wa miaka mitano,kina Mama wakati wa kujifungua,Wagonjwa wenye Saratani, Sikoseli, Virusi Vya UKIMWI na magonjwa wengine na wahanga wa ajali.

Naye Mhamasishaji wa damu salama na Mhudumu wa Afya ngazi ya jamii wa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma Rehema Kassim Mwegeru amezitaja sifa za mtu anaeweza kuchangia damu kuwa ni yeyote, mwanamke au mwanaume mwenye umri usiopungua miaka 18 na usiozidi miaka 65,uzito usiopungua kilo 50 na kwamba kwa mwanamke asiwe mjamzito au anaenyonyesha.

Amesema mwanamke anaweza kuchangia kila baada ya miezi 4 na Mwanamme kila baada ya miezi 3 na kufafanua kuwa uchangiaji damu unawezesha kupima afya bila malipo yoyote, ukichangia damu utapimwa kundi la damu, wingi wa damu, shinikizo la damu, Kaswende na Homa ya Ini B&C

“Uchangiaji damu unapunguza madini chuma mwilini ambapo yakizidi yanaweza sababisha mapigo ya moyo kuongezeka, mwili kujisika kuchoka n,k. Pia kwa kupunguza madini chuma mwilini inasaidia kuzuia uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo na ini,”amesema

Huku mchangia damu aliyetajwa kuwa na kundi la damu adimu,Dotto Faris Mukama amezitaja faida za kuchangia damu  ni tendo la upendo na kishujaa, unaokoa maisha ya watu na kwamba  Chupa moja inaweza kuokoa maisha ya hadi watu watatu.

Pamoja na hayo amewatoa wasiwasi wengine na kueleza kweli kuhusu kuchangia damu kuwa hakuna madhara yoyote na kwamba , mchangiaji damu hupimwa uzito, wingi wa damu, shinikizo la damu na pia ataulizwa maswali kuhusu maisha ya kila siku.

“Chupa moja ya damu inaujazo wa mililita 450 (ni sawa chupa moja ya soda ya kawaida na zaidi kidogo),asilimia 1 ya watanzania wakiamua kuwa wachangiaji wa damu wa kujirudia uhaba wa damu utaisha.

Pamoja na mambo mengine kauli Mbiu ya Siku ya Mchangia Damu Duniani inasema: Kuchangia Damu ni Kitendo cha Mshikamano, Tuungane Kuokoa Maisha ambayo  inaonyesha jukumu la uchangiaji wa damu kwa hiari linavyochangia  katika kuokoa maisha ya wahitaji na kujenga umoja ndani ya jamii.