Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,amemuelekeza Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa,kuongeza saa 24 za uokoaji katika jengo lililoporomoka eneo la Kariakoo.
Rais Dkt. Samia, ametoa maelekezo hayo,Novemba 19,2024,wakati akizungumza kwa njia ya simu na Waziri Mkuu Majaliwa, kuhusiana na zoezi la uokoaji eneo la Kariakoo jijini Dar-es-Salaam.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninatambua utaratibu wa uokoaji una muda maalum wa saa 72,mpaka kusitisha zoezi hilo. Binafsi nina matumaini kuwa Mwenyezi Mungu anaweza akatenda miujiza yake na kuweza kuwanusuru ndugu zetu wengine ambao bado wamenasa kwenye jengo hilo,amesema Dkt Samia na kuongeza:
“Ninakupa maelekezo ya kutositisha zoezi la uokoaji na kuongeza muda wa saa 24 zaidi,ili kuwapambania ndugu zetu ambao tunaamini bado wako hai,”.
Aidha,Dkt. Samia,ametoa pongezi kwa vikosi vyote na wananchi wote wanaopambana kuokoa maisha ya ndugu zetu katika zoezi hilo.
“Ninaomba ufikishe salamu zangu, na uwaeleze kuwa natambua na nina wathamini sana. Wameonesha utu, uzalendo na uchapakazi wa hali ya juu.Hivyo nawatia moyo na kuwapa nguvu ya kuendelea kuwapambania ndugu zetu,kwani ninyi ni mashujaa wa taifa letu,”.
Hivyo amewaombea kwa Mungu awalinde na kuwapa nguvu muda wote wakiwa wanateleleza jukumu hilo kubwa na la kizalendo.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia amewasihi wananchi, ndugu na jamaa kuendelea kuwa na subira.
“Na kama taifa tuendelee kuwaombea ndugu zetu na wapiganaji wetu ili tufanikishe zoezi hili kwa mafanikio.Mwenyezi Mungu tunakuomba utufanyie wepesi kwenye zoezi hili,”.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam