Na Mwandishi Wetu, Pemba
https://www.instagram.com/p/DO2kF5LCIus/?utm_source=ig_web_copy_link
MGOMBEA urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi wa Pemba na Watanzania kwa ujumla kutokubali kuchokozeka wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu.


Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM, ilieleza hayo ikimnukuu Dkt. Samia wakati akihutubia maelfu ya wananchi katika Viwanja vya Gombani ya Kale, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba, alisema serikali imejipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu.
“Niwaombe sana ndugu zangu, kipindi hiki ni kipindi ambacho wengine wanakitumia kuchokozana. Msichokozeke. Mimi kama mama, dada na bibi yenu nachokozwa sana, lakini sichokozeki. Hivyo nawaomba sana msichokozeke,” alisema Dkt. Samia.



Alisisitiza kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita, serikali imefanikisha kudumisha amani, hali iliyoiweka Tanzania katika mazingira ya utulivu wa kisiasa na kiusalama.
“Ndani ya miaka mitano yote hamjasikia vurugu ndani ya nchi hii. Hata waliovuka mipaka na kuleta vurugu tuliwashughulikia na hawajathubutu kurudi tena. Tusivunje amani kwa sababu ya uchaguzi,” alionya.
Aidha, aliwahakikishia wananchi kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga vyema kulinda nchi katika kipindi chote cha uchaguzi. “Hakutakuwa na vurugu, tokeni kwa wingi mkapige kura na msirudi nyuma,” alisisitiza.



Dkt. Samia pia alitoa ahadi za maendeleo kwa wananchi wa Pemba endapo atapewa tena ridhaa ya kuongoza, ikiwemo kujenga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Pemba, kukamilisha barabara ya Chake–Mkoani, kujenga Bandari ya Wete kwa mkopo kutoka Korea, pamoja na kukamilisha barabara saba muhimu ndani ya kisiwa hicho. Alimalizia hotuba yake kwa kusisitiza mshikamano wa kitaifa na kueleza kwamba “hakuna jambo lisilozungumzika,” akiwataka Watanzania kushiriki uchaguzi kwa amani, kisha kusubiri matokeo bila kuvuruga utulivu wa taifa.





https://www.instagram.com/p/DO2kF5LCIus/?utm_source=ig_web_copy_link

More Stories
Kihongosi amtaka mkandarasi kuwalipa vibarua stahiki zao
DC Mbozi afuturisha wananchi, asisitiza mshikamano na Umoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Nina imani mubna utendaji kazi wa ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria