November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Samia maboresho ndani ya Jeshi la Polisi,utawala bora umeleta utulivu wa. kisiasa

George Mwigulu, Timesmajira Online,Katavi

Rais Samia Suluhu Hassan, amesema maboresho yaliyofanywa ndani ya Jeshi la Polisi,yameimarisha utawala bora.

Amesema hali hiyo imeleta amani na utulivu wa kisiasa nchini kwani maboresho hayo ni utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai na ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 sura ya pili inaelekeza serikali kujega mazingira bora kwa Jeshi la Polisi.

Rais Dkt Samia ameeleza hayo wakati akizindua jengo la thamani ya bilioni 1.4 la Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi Julai 14, 2024,ambapo ameweka wazi kuwa jengo hilo ni moja ya majengo mengi yenye hadhi ya kufanana ambayo yamejengwa nchini.

“Niwapongeze Jeshi la Polisi wanatekeleza yale mapendekezo ya tume lakini wanatekeleza maelekezo yangu na sasa kama mnavyoona pilikapilika za kisiasa zinaendelea na nchi imetulia kabisa,” amesema Rais Dkt Samia.

Ameeleza kuwa Januari mwaka jana aliunda tume ya kuangalia uboreshaji wa miundombinu ya utendaji na mazingira ya kufanyia kazi kwa taasisi zote zinazoshughulikia haki jinai jambo ambalo limefanywa kwa ufanisi na kutoa taarifa na mapendekezo ambayo ni pamoja na kuboresha Jeshi la Polisi.

Serikali imetenga fedha nyingi za kufanya maboresho ndani ya polisi ambapo uzinduzi wa jengo hilo na majengo mengi ambayo yamezinduliwa na yanayosubiliwa kuzinduliwa ni katika utekelezaji wa mapendekezo ya tume ya haki jinai.

“Nieleze faraja yangu leo kuja kufungua jengo hili la ofisi ambayo itatumika na Kamanda wa Polisi Mkoa pia idara na vitengo vyote vya jeshi la polisi,”amesema Rais Dkt Samia.

“Ukiangalia jengo hili tumetimiza mapendekezo yote ya ile tume kwanza kuweka mazingira mazuri ya kufanyia kazi jeshi la polisi pia kuweka vitendea kazi. Na humu ndani nimeoneshwa mbali na mambo mengine kuna kamera zitakazo angalia usalama wa nje ya jengo na utendaji kazi wa mambo yanayotokea ndani ya jengo,”.

Pia amefafanua kuwa licha ndani na nje ya jengo kuwa na kamera lakini amesisitiza umuhimu wa jengo hilo kusomana na taasisi zingine za Jeshi la Polisi zilizopo mkoani humo.

Ametoa tahadhari kuwa na jengo zuri ni namna moja lakini utendaji kazi ni jambo jingine hivyo licha ya kumpa hongera Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa kupata jengo hilo amesisitiza linapaswa kutunzwa ili lidumu kwa miaka mingi na kuepuka aibu baada ya mwaka mmoja kamera kushindwa kufanya kazi na jengo kuwa na sura mbaya.

Aida amewaomba wananchi wa Mkoa wa Katavi kushirikiana na Jeshi la Polisi kutunza amani na utulivu ndani ya Mkoa ingawa hauna matukio mengi ya kihalifu lakini una mchanganyiko wa watu wengi.

“Tunapoufungua Mkoa huu kwa safari za ndege, barabara na usafiri wa majini mchanganyiko wa watu utakuwa mkubwa sana kutoka nje na ndani ya nchi yetu kwaio niwaombe sana kuhakikisha mnashirikiana na jeshi la polisi kutunza amani na utulivu” Amesema.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Hamad Masauni amesema jengo hilo ni sehemu ya vituo 12 vilivyojengwa kwa ngazi ya mikoa.

Masauni amesema kuna vituo ngazi ya mikao ofisi za makamada wa mikoa (RPC) sita vimekamilika Tarime Rorya vinasubilia kuzinduliwa na katika maeneo mengine akitolea mfano Mkoa wa Singida na Njombe vimeshaziduliwa tayari.

Waziri huyo amesema kuwa uwezeshaji wa makazi ya askari wamejenga nyumba nyingi nchini chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia ambapo sio Polisi pekee bali na vyombo vingine vyote kama vile Zimamoto,Uhamiaji na Magereza kuna maboresho ya miundombinu ili kuhakikisha mazingira yanakuwa bora ya huduma kwa wananchi sio kwenye majengo tu bali na vitendea kazi.

Mkadiriaji wa Majenzi, Aisha Tuwa awali akisoma taarifa kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan juu ya ujenzi wa jengo hilo la Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi amesema kuwa ujengo hilo limegharimu fedha bilioni 1.4.

Aisha amesema kuwa ukubwa wa jengo hilo ni mita za mraba 1438 likuwa na mgawanyiko wa sakafu nne na vyumba vya ofisi 33 huku likiwa limefungwa mifumo ya kisasa ya kamera.