May 17, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Samia ahimiza wananchi kujitokeza kujiandikisha


‎Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan,amewaasa watanzania kujitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao Ili waweze kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura kuchagua viongozi wanaoona wanaweza kuwaletea maendeleo katika maeneo yao na Taifa kwa ujumla.

‎Dkt.Samia ameyasema hayo Leo Mei 17,2025 Chamwino mkoani Dodoma muda mfupi mara baada ya kuboresha taarifa zake na kupata kitambulisho Cha mpiga kura.

‎”Kila mtu ana haki ya kikatiba ya kupiga kura kuchagua viongozi,hivyo kutoshiriki katika mchakato wa kujiandikisha au kuhuisha taarifa kwenye Daftari la Kudumu la Mpiga Kura ni sawa na mtu kujinyima haki yake ya kikatiba kwa hiari, jambo ambalo siyo uzalendo.”amesema Dkt.Samia na kuongeza kuwa

‎“Ukikataa kujiandikisha, unakosa nafasi ya kumchagua kiongozi unayemtaka,”

‎Amesisitiza kuwa kila raia ana wajibu wa kuhakikisha anatumia haki yake ya kupiga kura kama mchango kwa Taifa.

‎Rais Samia amesema kutokana na umuhimu wa kujiandikisha, ameamua kushiriki zoezi hilo akiwa kama mkazi wa Chamwino, ambapo pia atapiga kura katika uchaguzi ujao.

‎Amesema kuwa amerekebisha taarifa zake ili kuhakikisha anakuwa tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi.

‎Aidha, amewakumbusha wananchi kuwa huu ni mzunguko wa pili na wa mwisho wa uandikishaji na uhuishaji wa taarifa.

‎“Baada ya awamu hii, hakutakuwa na nafasi nyingine ya kujiandikisha. Hivyo basi, tumieni fursa hii kwa uzalendo na kwa manufaa yenu wenyewe,” ameongeza.

‎Rais Samia aliwahimiza wananchi kuwa wavumilivu pale changamoto zinapojitokeza katika vituo, akisisitiza kuwa Serikali imeweka mipango madhubuti kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma stahiki.

‎“Tuonyeshe uzalendo kwa vitendo. Tujitokeze kwa wingi, tuhimize wengine, na tusisite kufika vituoni,” alihimiza.

‎Zoezi la uandikishaji na uhuishaji linaendelea katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.