December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Nyansaho achangia Mil.20 ujenzi Zahanati ya Ring’wani, Serengeti

Na Fresha Kinasa, TimesMajiraOnline, Mara

MKURUGENZI wa Maendeleo ya Biashara Benki ya Azania Tanzania, Dkt. Rhimo Nyansaho amechangia kiasi cha Shilingi Mil.20  kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Ring’wani kilichopo  Kata ya Ring’wani Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.

Dkt.Nyansaho ametoa kiasi hicho kilichowasilishwa na mwakilishi wake ambaye ni  Katibu Tawala Wilaya ya Serengeti, Angelina Marco katika harambee iliyofanyika jana (Dicemba 23, 2024) kijijini hapo, ambapo wananchi, wadau wa maendeleo, na viongozi wa serikali wameshiriki harambee hiyo.

Katika harambee hiyo zaidi ya shilingi milioni. 84, zimepatikana, ambapo Dkt. Nyansaho ametoa shilingi milioni 20 taslimu,  Serikali ikitoa ahadi ya  milioni 50, huku zaidi ya  shilingi milioni 14.5, zikitolewa na Umoja wa Maendeleo Ring’wani ambayo imewekwa kwenye akaunti ya ujenzi wa Zahanati hiyo.  

Akizungumza katika harambee hiyo kwa niaba ya Dkt. Nyansaho, Katibu Tawala wa Wilaya ya Serengeti, Angelina Marco amesema, malengo ya serikali ni kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati. Hivyo ameupongeza Umoja wa Maendeleo Ring’wani unaoundwa na wasomi mbalimbali  waliozaliwa kijijini hapo  kwa uamzi wa  kuhamasishana na  kuchangia fedha kuhakikisha kijiji  hicho  kinapata zahanati. 

Pia amesema serikali itatoa fedha Shilingi Mil. 50 kusaidia ujenzi wa zahanati hiyo, huku pia akisema fedha hiyo inapaswa kutumiwa vyema kuwezesha ujenzi huo ili mwakani mwezi machi  2025, iwe imekamilika.  

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti,  Ayubu Mwita Makuruma amesema kuwa ujenzi wa zahanati hiyo ni muhimu kwa ajili ya Wananchi kuwahidumia.

Amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita,  serikali imetoa fedha zaidi ya Shilingi Bil.  50, ambazo zilitekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuleta mapinduzi chanya kwa Wananchi wa Wilaya hiyo. 

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Serengeti Mrobanda Japan Mkome amewataka Wasomi kujenga utamaduni wa kusaidia Jamii  kupitia elimu, ujuzi na vipato vyao na kuachana na tabia ya ubinafsi kwani kufanya hivyo pia ni baraka na neema kwa Mwenyezi Mungu. 

“Niwaombe Wasomi mjenge tabia ya kutumia elimu  zenu,  maarifa, ujuzi na vipato vyenu ambavyo Mungu anawajalia kusaidia Jamii hasa kujenga miradi ambayo itawagusa moja kwa moja Wananchi na kutatua kero zao mbalimbali. Kwa Wasomi wa hapa Ring’wani mmeonesha mfano bora kuamua kujenga Zahanati ambayo itakuwa kumbukumbu njema kwa Jamii.” amesema Japan.

Awali akisoma risali ya ujenzi wa Zahanati hiyo  Dkt.  Genchwere Makenge  amesema kuwa Kijiji Cha Ring’wani kina jumla ya Wananchi 2,727, ambapo wanawake ni 1,388, na wanaume ni 1,339, na Kijiji hicho kina Vitongoji vitatu. 

Amesema ujenzi wa Zahanati ya Kijiji hicho ulianza mwaka 2015, kwa kujenga Msingi na mwaka 2016, na 2017 ujenzi wa boma ulikamilika chini ya uongozi wa Kijiji uliokuwepo kipindi hicho. 

Amesema kuwa makisio ya awali ya gharama za ujenzi wa Zahanati hiyo ni kupata Shilingi Mil.  100, kwa ajili ya kukamilisha jengo la  (OPD) choo cha wagonjwa na kichomeo Cha taka. Huku akisema kukosekana kwa Zahanati Kijijini hapo kumekuwa kukisababisha wanawake wanaojifungua kutembea umbali mrefu kwenda kupata huduma katiki Vijiji vya  Kemugesi au Kenyana. 

“Wakati mwingine wanabaguliwa kupata huduma kwa sababu wao sio Wakazi wa Vijiji hivyo. Hatua hiyo imekuwa ikipelekea pia kina mama kutowapeleka chanjo Watoto wao na wakati mwingine Watoto kutopata chanjo kwa wakati kutokana na umbali na tunafahamu mtoto asipopata chanjo madhara yake ni mabaya.”amesema Dkt Makenge.

Rhoda James ni Mkazi wa Kijiji cha Ring’wani amesema kuwa Wananchi wa Kijiji hicho shauku yao ni kupata Huduma za Afya Kijijini hapo, hivyo kukamilika kwa Zahanati hiyo utakuwa mwarobaini wa kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu  kwenda Vijiji  Jirani kufuata Huduma.