
Na Joyce Kasiki,Timesmajira online
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, amesema kuwa Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) ni mhimili muhimu unaoshikilia mchakato mzima wa uandishi, urekebishaji na ufasili wa sheria kuu na sheria ndogo nchini.
Dkt.Ndumbaro ametoa kauli hiyo alipotembelea banda la OCPD katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es Salaam.
Dkt. Ndumbaro amesema kuwa bila uwepo wa OCPD hakuna sheria inayoweza kutungwa bungeni, kurekebishwa wala kufasiliwa kwa lugha nyepesi kwa wananchi. “Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria ni mhimili muhimu sana katika mchakato wa utungaji sheria. Bila ofisi hii hakuna sheria itakayokwenda bungeni kutungwa, wala kufanyiwa marekebisho. Pia hakuna sheria ndogo itakayotungwa bila kupitia ofisi hii,” alifafanua Waziri.
Amefafanua kuwa , “Endapo ofisi hii haitakuwepo, Mahakama nayo itapata changamoto katika kutoa haki kwa kuwa ni OCPD inayotufahamisha ipi ni sheria sahihi na ya lini, sambamba na kutafsiri sheria kutoka Kiingereza hadi Kiswahili ili wananchi wazielewe.”
Kwa mujibu wa Waziri, hadi kufikia tarehe 30 Juni mwaka huu, ofisi hiyo ilikuwa imeshafasili jumla ya sheria 300 kati ya 446. Aliongeza kuwa katika mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga bajeti ya kutosha kuwezesha OCPD kukamilisha kazi ya ufasili wa sheria zote nchini.
Dkt. Ndumbaro alieleza kuwa OCPD inatoa mchango mkubwa katika uchakataji wa miswada ya sheria inayowasilishwa bungeni, kuhakikisha inazingatia misingi yote muhimu ya utungaji wa sheria kabla ya kuwa sheria kamili.
Awali, akizungumza na Waziri, Mwandishi wa Sheria kutoka OCPD, Bw. Philemon Mrosso, amesema kuwa ofisi hiyo ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha ufasili wa sheria zilizobaki pamoja na kanuni zake, ili ziwe tayari kwa matumizi kabla ya Oktoba mwaka huu.
“Mhe. Waziri, tunashiriki maonesho haya kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi na wadau wa sheria kuhusu mchakato mzima wa utungaji sheria, pamoja na kuwaeleza majukumu ya ofisi yetu ili waweze kufahamu namna ya kufikia huduma zetu,” ameeleza Bw. Mrosso.
Aidha, amesema kuwa OCPD hupokea maoni kutoka kwa wananchi na wadau kuhusu sheria mbalimbali, na kuwaelekeza njia sahihi za kuwasilisha mapendekezo yao kupitia wawakilishi wao bungeni, ili kuimarisha ushiriki wa jamii katika mchakato wa utungaji sheria nchini

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi