Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dkt.Damas Ndumbaro amesema serikali itaendelea kutoa fursa kwa wawekezaji kwenye sekta ya utalii pamoja na kuendelea kuboresha huduma za kitalii nchini ikiwemo upatikanaji wa leseni ya shughuli za utalii kwa uharaka zaidi pamoja na mifumo ya malazi.
Dkt.Ndumbaro amesema hayo jijini hapa leo wakati akikabidhi vyeti kwa wawekezaji waliokidhi vigezo na kufanikiwa kupata maeneo ya uwekezaji katika maeneo mahiri (SWICA), yanayosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA),ambao ni kampuni nne ya Green Nile Safari LTD,Grumet Services Ltd,Mwiba Holding LTD,na kampuni ya ndani ya Mkwawa Hunting Safari.
Hivyo amewasisitiza wawekezaji wazawa pamoja na wa kigeni kulinda na kutangaza utalii na maeneo ya uhifadhi na vivutio hapa nchini, katika maeneo waliyopewa kuwekeza kwa kushirikiana na serikali.
Pia amewataka wawekezaji wazawa na wa kigeni kuchangamkia fursa za uwekezaji wa uwindaji na utalii zilizopo nchini huku akisema fursa hizo zina manufaa kwao kama wawekezaji na pia zinamanufaa kwa Serikali.
Pia Waziri Ndumbaro ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wawekezaji wa kigeni kuwekeza nchini, akiitaja Tanzania kuwa ni salama, yenye amani na demokrasia na kwamba Wizara anayoiongoza imefungua milango kwa wawekezaji wote kuja kuwekeza nchini.
“Sisi Kama Wizara ya Maliasili na Utalii, falsafa yetu ni moja tu, mteja ni mfalme. Ndio maana mimi, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, tuko tayari kukutana na mwekezaji wa aina yoyote yule, muda wowote ule kujadili changamoto zozote zile, milango iko wazi,”amesema.
Pamoja na hayo Dkt.Ndumbaro, ameipongeza TAWA kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za Taifa akisema kuwa Taasisi hiyo ni changa kuliko Taasisi zingine lakini wanafanya kazi ngumu na mazingira magumu zaidi ila wanafanya vizuri.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi TAWA,Meja Jenerali Mstaafu Hamis Semfuko, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa kuipatia TAWA fedha kiasi cha Shillingi Billioni 12.9, ili kutekeleza miradi ya miundombinu ya Utalii kupitia kampeni ya Maendeleo ya Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19.
Amesema miradi hiyo inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye maeneo ya SWICA huku akithibitisha kuwa TAWA imeweka mipango madhuhuti, kuhakikisha miradi yote ambayo imekusudiwa kutekelezwa kwa kutumia fedha hizo inatekelezwa ndani ya muda uliopangwa na kwa ubora uliokusudiwa.
Wakizungumza mara baada ya kukabidhiwa vyeti hivyo Mwenyekiti wa bodi ya Grumeti Reserves Ltd Prof. Hussein Hassan Sosovele amesema kampuni ya Grumeti inashukuru kupata cheti cha umiliki wa kitalu cha Grumeti cha SWICA na inaahidi kuyatekeleza yote yaliyosemwa kwenye andiko la mradi huku akiomba serikali kukamilisha mapema mchakato wa kupata kitalu kilichobaki cha Ikorongo.
Naye mwakilishi wa kampuni ya Mkwawa Hunting Safari Bw. Benson Kibonde, ameishukuru Serikali kwa juhudi inazofanya kuhakikisha shughuli za Uhifadhi zinapata mwelekeo Kama wananchi wanavyotazamia huku akihaidi kuwa kama mmoja wa wazawa, watatumia akili na nguvu zao zote katika masuala mazima ya uwekezaji katika tasnia ya Utalii na Uhifadhi wa Wanyamapori, ili kuweka mchango wao katika ukuaji wa sekta ya utalii nchini.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais