Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Balozi,Dkt.Emmanuel Nchimbi amewatangazia vita wanachama wa chama hicho ambao wanataka kugombea nafasi mbalimbali kwa kutoa matamko ya kutaka kuwa wagombea pekee na kuwachafua wabunge waliopo sasa na kutoa rushwa kwa wajumbe.
Balozi Dkt.Nchimbi amesema kuwa wapo baadhi ya wanachama ambao wanatamani kuwa wagombea kuanzisha tamaduni ya kutengeneza makundi ya kutoa matamko ya kuwataka baadhi ya wanasiasa ndani ya chama hicho kuwa wagombea pekee jambo ambalo halikubaliki ndani ya Chama na wanachama wa aina hiyo wataenguliwa mapema majina yao.

Katibu Mkuu huyo amesema hayo jijini hapa leo,Februari 19,2025 alipokuwa akifungua mafunzo kwa makatibu tawi,kata,wilaya na Mkoa katika Mkoa wa Dodoma.
“Wapo wanachama watakao gombea na watakao hamasisha matamko kwenye maeneo yao ili wawe wagombea pekee wagombea hao watahamasisha kuenguliwa kwa majina yao kirahisi.
“Umeanza utaratibu wa watu wanaotamani kuwa wagombea kutengeneza matukio mbalimbali kwenye maeneo yao mtu anasema kumbukumbu ya marehemu bibi yake aliyefariki mwaka 70 anaalika wajumbe 3000 na kumbukumbu ya mama yake anatoa na posho kwenye kumbukumbu ya mama yake?alihoji Dkt.Nchimbi.
Ameeleza kuwa kuna mchezo wa mtu anasema anafanya sherehe ya kuzaliwa kwake anaalika watu 900 anatoa na posho na waalikwa wote wamevaa na sare CCM.
“Sasa hapo imezaliwa CCM umezaliwa wewe?lakini kama wanataka wagombee na visingizio vya kumbukumbu ya kuzaliwa,kukumbuka marehemu bibi na kumbukumbu ya ndoa waendelee tu tutawafuatilia,”amesema Dkt.Nchimbi.
Kiongozi huyo amesema kuwa kutokana na kuwepo kwa matukio hayo uongozi wa CCM umeanza kufuatilia matukio ya aina hiyo na iwapo uongozi utajiridhisha kuwa kuna mgombea anafanya vitendo vya kutoa rushwa au kusingizia kufanya sherehe na matamko mgombea huyo hataweza kupenya.
Dkt.Nchimbi amewataka makatibu ambao watakuwa sehemu ya usimamizi wa uchauzi uhakikisha wanafuatilia matukio na uweka rekodi vizuri ili pale itakapo bainika kutokea mambo hayo atakayekuwa anagombea achujwe mapema.


Katika hatua nyingine amesema kuwa uchaguzi ndani ya Chama hicho unalenga kuwasimamisha wagombea ambao wanakubalika katika jamii na siyo wale ambao wanaingia madarakani kwa kutoa rushwa.
Ameendelea kuonya kuwa wapo watu ambao wameanza kampeni za kuwatoa majimboni wagombea wabunge waliopo kwenye maeneo yao na kampeni chafu.
“Watu wanatengeneza mpaka fulana mtu anapeleka kwenye jimbo fulana 5000 zimeandikwa “Tokomeza Gavu Mpanda”sasa wewe ni mwanaccm kweli unamchafua mwenzako Tomkomeza hii ni UKIMWI?Mwenzako unamtokomeza halafu wanaamini kabisa kwenyw vikao vya uteuzi vya chama chetu utagawa fulana za namna hiyo kwenye jimbo halafu sisi tutakupitisha wewe kuwa mgombea wa chama chetu,hiyo haitatokea tunataka kuwa na chama ambacho wanaccm wote wanajisikia kuwa ni ndugu,
“Wanaccm wote hawafanyi matukio ya kuumiza mwili au moyo wa mtu,”amesema Dkt.Nchimbi.
Amesema wao hawakasiriki viongozi wao kupata posho,wanafurahi lakini wanaotoa hiyo posho haitakuwa kisingizio cha kuteuliwa kwani unaonekana mtoa rushwa huwezi kuwa kiongozi wa chama hicho.
“Kwasababu kwanza uzoefu umeonesha watu wanaogawa fedha kirahisi fedha zenyewe wametuibia sisi wenyewe kwahiyo wakiturudishia siyo tatizo kubwa sana,”amesema Dkt.Nchimbi
More Stories
Tanzania yajivunia ushirikiano kati yake na Kuwait
Mbunge Mavunde akabidhu mradi wa Shamba kwa wanawake wafanyabiashara wadogo Dodoma
Wasira aihakikishia Marekani uchaguzi nchini kuwa wa huru na haki