Na Penina Malundo, Timesmajira.
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM Taifa Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi amepokelewa Mkoa wa Lindi kwa vifijo na nderemo akitokea Mkoani Mtwara akiwa Mnazi mmoja amezungumza na mamia ya wananchi waliokuwa wakimsubiri.
Balozi Nchimbi akijibu kero za wananchi wa Mkoa wa Lindi amesema wananchi hawatapata mafanikio ya kweli kama wakiendelea kuuza korosho ghafi.
“Lazima tubangue wenyewe ili tupate faida sasa natoa maelekezo kwa Mawaziri wa kilimo na Viwanda na Biashara ,kuhakikisha Korosho yote ibanguliwe hapa hapa nchini ili kuongeza thamani ya zao letu hili na kama viwanda vijengwe ili kukuza uchumi wetu,”amesema.
Amesema endapo ubanguaji wa korosho utafanyika nchini utasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua tatizo la kudumu la changamoto ya kuuza Korosho ghafi na bei kuwa chini.
“Sisi kama Chama cha Mapinduzi tutalisimamia na kuhakikisha linaingia katika ilani ya Chama cha Mapinduzi na kuona kwamba tunawapa wakulima wetu ukombozi wa moja kwa moja katika kutatua changamoto wanazopitia katika zao hili,”amesema.
Aidha Balozi Dkt.Nchimbi alizungumzia suala la amani na ushirikiano nchini,amesisitiza wananchi na wanaccm kuhakikisha wanadumisha amani na mshikamano uliopo nchini.
“Naomba nisisitize na sitaacha kusisitiza hili kwamba umoja na mshikamano nchini kwetu havijadondoka kutoka mbinguni bali Mungu alijalia kupata viongozi wazuri akiwemo Baba yetu wa Taifa, Mwl Julius Nyerere na wenzake ambao walifanya kazi kubwa ya kujenga umoja katika nchi yetu,”amesema na kuongeza
“Marais wote waliopita ambao ni wenyeviti wa Chama chetu , walienda hatua kwa hatua kupokezana na kukabidhiana nchi yenye amani na umoja,hivyo jukumu letu ni kuhakikisha watoto wetu na wajukuu zetu tunawarithisha nchi yenye umoja na mshkamano na yenye utulivu,”amesema.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito