March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Nchimbi ahimiza viongozi wa dini kuombea amani

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Kigoma

MGOMBEA Mwenza wa kiti cha Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amewahimiza viongozi wa dini nchini, kuendelee kuiombea nchi amani, upendo, umoja na mshikamano.

Dkt. Nchimbi ameyasema hayo Oktoba 12, 2025,uwanja wa shule ya msingi Kakonko, mkoani Kigoma,akiendelea na mikutano yake ya kampeni za kukinadi Chama Cha Mapinduzi na kuwaombea kura wagombea wa chama hicho ikiwemo wa urais,Wabunge na Madiwani.

Amesema,chama hicho kitaendelea kutimiza wajibu wake wa kuhakikisha kinasimamia yale iliyoahidi kama umoja na mshikamano, ili kuendelea kuwa nchi ya haki na inayojali wananchi wake.

“Kwa niaba ya CCM,tunawashukuru viongozi wote wa dini zote nchini, ambao wamekuwa wakielekeza juu ya umoja na mshikamano kama kitu cha msingi kuliko vyote, tunawasihi waendelee kuiombea nchi yetu na sisi kwa nafasi yetu kama Chama cha Mapinduzi, tutaendelea kutimiza wajibu wetu,”amesema Dkt. Nchimbi.

Pia amesema, endapo chama hicho kitashika dola kitaendelea kupeleka miradi ya maendeleo kwa wananchi wa Kakonko katika sekta ya mbalimbali ikiwemo elimu, afya,kilimo na miundombinu ya barabara.

Hata hivyo amesema, katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali chini ya CCM itahakikisha inaendelea kuwaboreshea mazingira rafiki wananchi kwa kuongeza shule za msingi nne,sekondari tatu,maabara 15 ili kuwarahisishia wanafunzi wa masomo ya sayansi, mabweni 10 na kuboresha shule zote za zamani kwa kuziongezea madarasa 107.

Huku katika afya inaboresha hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko kwa kuongeza majengo, vitendea kazi na madaktari bingwa, ujenzi wa vituo vya afya vitano na zahanati tisa.

Kwa upande wa kilimo zitaongezwa skimu za umwagiliaji tatu,ujenzi wa visima na mabwawa makubwa ya umwagiliaji, kutoa mafunzo kwa maofisa ugani na kuwapatia vitendea kazi, ujenzi wa maghala na vituo vya kukusanyia nafaka.

Chanjo na dawa zitaendelea kutolewa.kwa mifugo,pia serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya wafanyabiashara kwa kuwawekea mfumo rasmi utakaowasaidia,kuimarisha diplomasia ya uchumi ili kuunga mkono juhudi za Dkt. Samia alizofanya katika nchi za jirani na kuendelea kuwa na uhusiano mzuri na kufanya biashara pamoja.

Sambamba na hayo, Dkt. Nchimbi, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, mwaka huu kupiga kura na kumchagua Dkt. Samia Suluhu Hassan, wabunge wa CCM na madiwani ili waendelee kuwaletea miradi ya maendeleo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.