Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online -Tanga
Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi ya siku tano mkoani Tanga ambapo atatembelea, kukagua, kuweka mawe ya msingi, na kuzindua miradi mbalimbali ya maendleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 758.
Mradi mkubwa wa umeme uliopo wilayani Handeni uliofikia asilimia 60 ni moja ya mradi ambao ataukagua huku ukielezwa kuwa utawezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wilaya za Handeni, Pangani na Korogwe.

Akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wazee wa Mkoa wa Tanga, Mkuu wa Mkoa huo, Balozi Dkt. Batilda Buriani, amesema ziara hiyo inalenga kukagua utekelezaji wa miradi, kusikiliza changamoto za wananchi pamoja na kutoa maelekezo ya kuboresha huduma kwa jamii.
Ambapo Waziri Mkuu huyo anatarajiwa kupokelewa leo Februari 13,2026 majira ya saa tatu asubuhi Mkata,wilayani Handeni, akitokea mkoani Pwani.
Akiwa katika Wilaya ya Handeni, Waziri Mkuu atakagua mradi mkubwa wa umeme utakaohudumia wilaya za Handeni, Pangani, na Korogwe, kisha atakagua na kufungua jengo la chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) na kuweka jiwe la msingi la ujenzi na kuzungumza na wananchi.
Baada ya hapo, msafara utaelekea wilayani Kilindi kukagua mradi wa tenki la maji na hospitali ya wilaya, kabla ya kuelekea Korogwe kwa ajili ya ukaguzi wa mradi mkubwa wa maji wa miji 28.
Batilda amesema Februari 15,mwaka huu Dkt.Nchemba atakuwa wilayani Mkinga kukagua ujenzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, kisha kuelekea jijini Tanga kukagua maboresho ya Bandari ya Tanga na kuzungumza na wananchi katika viwanja vya Lamore.
Sambamba na hayo atakagua mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi (EACOP) kutoka Ohima nchini Uganda hadi eneo la Chongoleani jijini Tanga pamoja na viwanda vya mifuko, kisha kuelekea Pangani kukagua daraja la mto Pangani na Muheza kukagua jengo la Halmashauri.
Februari 17,2026, Waziri Mkuu atahitimisha ziara yake wilayani Lushoto kwa kuweka jiwe la msingi katika hoteli ya kitalii ya Java Boutique pamoja na kuzindua kituo cha kutengenezea oxygen katika hospitali ya wilaya na kukagua shule ya Amali Mlalo kabla ya kuelekea mkoani Kilimanjaro.

Kwa upande wao, wazee wa Mkoa wa Tanga wameeleza matarajio yao kuhusu ujio wa Waziri Mkuu, wakisema wanaamini ziara hiyo itasaidia kutatua changamoto mbalimbali na kuharakisha maendeleo ya mkoa huo.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama