*Azindua meli hiyo, aisisitiza TASHICO kuimarisha usalama
Mkurungezi TASHICO asema meli hiyo ni kubwa ndani ya Ziwa Victoria
Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Mwigulu Nchemba,ametaka ujuzi uliopatikana wakati wa utekekalezaji wa mradi wa ujenzi wa meli ya MV.New Mwanza uendelea kutumikia katika miradi mingine ya meli.
Dkt.Nchemba,amezungumza hayo Januari 23,2026 mara baada ya kuzindua meli ya MV.New Mwanza,yenye uwezo wa kusafirisha abiria 1200,tani za mizigo 400, magari makubwa matatu na madogo 20, uliofanyika bandari ya Mwanza Kusini,jijini Mwanza.

“Menejimenti ya Wizara ya Uchukuzi na Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO),hakikisheni huu ujuzi uliopatikana kwenye mradi huu,unaendelezwa katika kutumika kwenye miradi mingine ya namna hii,”amesema Dkt.Nchemba na kuongeza:
“Natambua kuna ujenzi wa meli unaendelea Ziwa Tanganyika ambayo na yenyewe itakuwa kubwa ukilinganisha na majira wa upande mwingine,na huku tumeunganishwa na majirani ambao ni ndugu zetu kwa muda mrefu,tunashirikiana nao kupitia miundombinu hii ambayo tumeijenga,”.
Pia ameitaka TASHICO kuhakikisha wanashirikiana na wadau wengine kuimarisha usalama wa usafiri majini ili kuwalinda wananchi.
“TASHICO hakikisheni meli hii inatunzwa ipasavyo,wanasema,’kitunze kidumu,ukiangalia mule ndani ni meli ya kisasa.Tuchukue hatua zinazostahili za kitaalamu vyombo vya majini,reli za kisasa na ndege havihitaji mazoea inataka ufuatishe ushauri wa kitaalamu kwa sababu hivyo ndivyo vilivyotengenezwa,”amesema Dkt Nchemba.
Sanjari na hayo ameitaka kampuni hiyo kuhakikisha usafiri wa majini unasaidia kukuza diplomasia ya majini,uchumi na amani baina ya Tanzania na majirani,huku akiwataka kuzingatia masuala ya bima kama sheria inavyoelekeza kwenye vyombo vya usafiri majini,angani na nchi kavu.
Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi,Profesa Makame Mbarawa,amesema,mradi wa ujenzi wa meli ya MV.New Mwanza umetumia gharama ya Dola za Kimarekani zaidi ya milioni 51.8 sawa na zaidi ya bilioni 120.56,umetekelezwa na Kampuni za GAS ENTEC CO. LTD na KANGNAM zote kutoka Korea Kusini, kwa kushirikiana na SUMA JKT.
Profesa Mbarawa amesema ushirikiano huo umewezesha uhamisho wa teknolojia na uzoefu kwa wataalamu wa nchini hapa.
“Wakati Serikali ya awamu ya sita inaingia madarakani, mradi huu ulikuwa umefikia asilimia 40 tu ya utekelezaji, huku mkandarasi akiwa amelipwa kiasi cha bilioni 40.6.Lakini Serikali imewezesha mradi huu kukamilika kwa kutoa kiasi chote cha fedha zaidi ya bilioni 79.9 kilichohitajika kukamilisha mradi,”amesema Profesa Mbarawa.

Sanjari na hayo Profesa Mbarawa,amesema Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi imefanya marekebisho ya meli za MV.Umoja (Ziwa Victoria) na MT Sangara (Ziwa Tanganyika) hali inayothibitisha dhamira yake ya kuboresha huduma za usafiri wa majini kote nchini.
“Tayari fedha zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha meli (shipyard) katika Ziwa Tanganyika,kitakachoongeza uwezo wa kitaifa wa kujenga na kukarabati meli, kupunguza utegemezi wa huduma za nje na kuzalisha ajira kwa wananchi,”amesema Profesa Mbarawa.
Awali akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi wa meli ya MV.New Mwanza Mkurugenzi wa Kampuni ya Meli Tanzania(TASHICO),Eric Hamissi,amesema lengo la mradi huo ni kutoa meli mbadala baada ya kuzama kwa meli ya MV.Bukoba mwaka 1996 pia unatimiza kikamilifu Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Uchaguzi ya mwaka 2020.
Hamiss amesema,MV.New Mwanza ni meli kubwa kuliko zote katika Ziwa Victoria,ina uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo, pamoja na magari makubwa 3 na magari madogo 20.
Pia ina urefu wa mita 92.6, karibu sawa na uwanja wa mpira wa miguu, na upana wa mita 17, ikiwa na kimo cha ghorofa nne ambapo meli hiyo imeundwa kwa viwango vya kimataifa.
“Meli hii ni ya kisasa ina vifaa na miundombinu ya hali ya juu kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa wasafiri. Inayo vifaa vya kisasa vya kuongozea meli na mwendokasi wa juu wa knots 16 kasi yake hii itaiwezesha meli kusafiri kati ya Mwanza na Bukoba kwa muda wa saa 6 tofauti na meli zilizopo zinazotumia wastani wa saa 8,”amesema Hamissi.
Pia amesema wametoa kipaumbele katika usafiri jumuishi katika meli hiyo ambapo imewekewa lifti (elevator) ambayo itawezesha watu wenye mahitaji maalum kupanda na kuteremka kutoka melini kwa urahisi.
Meli hii ina madaraja sita ambapo Daraja la Uchumi (Economy Class) lina uwezo wa kubeba abiria 834, Daraja la Biashara (Business Class) lina uwezo wa kubeba abiria 200, Daraja la Pili kulala (Second sleeping Class) lina uwezo wa kubeba abiria 100, Daraja la Kwanza lina uwezo wa kubeba abiria 60, Daraja la Hadhi ya juu (Executive Class) lina uwezo wa kubeba abiria 4 na Daraja la watu mashuhuri (VIP Class) lina uwezo wa kubeba abiria 2.
“Mradi huu ulianza kutekelezwa Januari 17,2019 baada ya mkandarasi kulipwa fedha za awali kwa mujibu wa mkataba na ulikamilika tangu Oktoba, 2025.Mradi huo ulitekelezwa katika chelezo kilichopo Bandari ya Mwanza Kusini, ulisimamiwa na Meneja mradi aliyeshikizwa TASHICO kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania, Kamandi ya Wanamaji, akishirikiana na Mtaalam Elekezi, Kampuni ya OSK Shiptech kutoka nchi ya Denmark,”amesema Hamissi.

Hata hivyo amesema,tayari meli hiyo imeshafanya jumla ya safari (voyage) sita kati ya Mwanza na Bukoba kupitia Kemondo na kupitia safari hizo jumla ya abiria 7,028 na tani 673 za mizigo.
“Meli hii inatarajiwa kuboresha hali ya usafiri kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, ikiwemo Mwanza, Geita, Kagera, Simiyu na Mara. Kwa sasa Kampuni inaendelea na utafiti wa kibiashara utakaowezesha kuongeza njia nyingine ikiwemo safari za nje ya nchi ikiwemo Uganda na Kenya.Inatarajiwa kuwa kiunganishi muhimu kwa Reli ya Kisasa ya SGR pindi ujenzi wake utakapokamilika kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza,hivyo kufungua fursa mpya za kibiashara na kiuchumi kwa taifa letu,”amesema.


More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi