March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Nanauka amewezesha mtaji binti mchoma mahindi

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Tabora

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana,Dkt. Joel Nanauka ameleta neema kwa kijana muuza mahindi ya kuchoma Hadija Seif mkazi wa Kata ya Ng’ambo, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora baada ya kumwezesha mtaji wa shilingi laki 3.

Dkt.Nanauka amemwezesha mtaji huo wakati akifungua Jukwaa la Vijana wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati vilivyopo mkoani Tabora, katika ukumbi wa chuo cha Utumishi wa Umma mjini hapa.

Ameeleza kuwa,jana akiwa katika pita pita zake mitaani baada ya kuwasili mjini Tabora alimuona dada mmoja akichoma mahindi na alipomuuliza mradi huo unamsaidiaje akasema kuwa unampatia kipato kidogo cha kutunza watoto wake.

Na alipomuuliza ndoto yake ni nini, akaeleza kuwa anatamani kuwa na biashara ya kuuza vyombo vya nyumbani na kuuza samaki wa kukaanga, ila mtaji hana na alipoulizwa anatamani kuwa na mtaji wa kiasi gani akasema shilingi 300,000.

“Sikujitambulisha kuwa mimi ni Waziri ila nilimwambia aje ukumbi wa Chuo cha Utumishi wa Umma kuna mkutano wa vijana, nikampa namba, na leo amekuja, njoo uchukue ule mtaji (shilingi laki 3) ukaendeleze biashara yako,”amesema Dkt.Nanauka.

Kwa upande wake Hadija Seif,ambaye mume wake alifariki, ameeleza kujawa na furaha isiyo kifani kwa kuwezeshwa kiasi hicho na mtu ambaye hakumfahamu, kumbe ni Waziri wa Vijana.

“Nakushukuru Waziri kwa upendo wako wa hali ya juu na kujali maisha ya vijana, ambao hawana matumaini yoyote ya kuinuka kiuchumi, hakika umenifuta machozi, Mwenyezi Mungu akubariki,”amesema Hadija.

Hadija ameeleza kuwa kiasi hicho kitamsaidia kuongeza mtaji wa kuchoma mahindi na kuanzisha biashara nyingine ya kukaanga samaki, kwani awali alikuwa na mtaji wa shilingi elfu kumi,akaanzisha biashara ya kuchoma mahindi.

Katika mkutano huo,Dkt.Nanauka amewataka vijana wote kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotangazwa na serikali ili kuwezeshwa mikopo nafuu isiyo na riba na kujikwamua kiuchumi.

Amesisitiza kuwa serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 200 kuwezesha vikundi mbalimbali vya vijana mikopo nafuu ili kuanzisha miradi yao pasipo kikwazo chochote.