January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.George Mwita kutoka Oxfam Tanzania akitoa mada.

Dkt.Mwita:Tuendeleze ajenda ya kilimo kwa matokeo bora

Na Godfrey Ismaely, TimesMajira Online

IMEELEZWA kuwa, kuendeleza ajenda ya kilimo, ufugaji, uvuvi kwa kushirikisha wadau mbalimbali nchini itasaidia kuharakisha maendeleo ya wazalishaji wadogo hapa Tanzania.

Hayo yamesemwa na Afisa wa Ushawishi kutoka shirika la Kimataifa lisilokuwa la kiserikali la Oxfam Tanzania, Dkt.George Mwita wakati akitoa mada katika warsha maalumu ya siku mbili iliyowakutanisha wahariri na waandishi wa habari za kilimo mkoani Dar es Salaam.

“Kilimo ni sekta muhimu katika maendeleo na uchumi wa Tanzania,kwani kinachangia fursa za ajira kwa zaidi ya asilimia 65, pato la taifa asilimia 30, bidhaa zinazouzwa nje ya Tanzania asilimia 30, malighafi ya viwanda nchini
asilimia 65 na kuendelea.

“Ndiyo maana Serikali ya Tanzania imekuwa ikiweka mikakati mbalimbali kama Mkakati wa Mendeleo ya Sekta ya Kilimo na Mkakati wa Maendeleo ya Sekta ya Mifugo ili kuhakikisha kwamba sekta ya kilimo inakua zaidi na
kuchangia ukuaji wa uchumi,”amefafanua Dkt.Mwita huku akiongeza kuwa,

Mafunzo hayo yalilenga kuiinua zaidi sekta ya kilimo kwa kutengeneza daraja baina ya Serikali, wadau mbalimbali zikiwemo asasi za kiraia, wakulima na wanahabari ambao wana jukumu la kuhakikisha wakulima wanapata taarifa zinazohusiana na sekta ya kilimo pamoja na kuhimiza Serikali kuweka sera rafiki zaidi kwa wakulima.

Katika mafunzo hayo mada mbalimbali zilijadiliwa na mapendekezo yatokanayo na warsha hiyo yatawafikia wadau walengwa ili kuweza kuimarisha zaidi sekta ya kilimo.

Shirika hilo lilianza kufanya kazi nchini Tanzania tangu miaka ya 1960 na wamekuwa wakitekeleza programu mbalimbali ikiwemo uwezeshaji wa wanawake, kukabiliana na umaskini, usawa pamoja na utawala sawa kwa wote programu hizo zinatekelezwa katika mikoa mbalimbali ikiwemo Shinyanga, Morogoro, Arusha na Dar es Salaam.

Dkt.Mwita ameongeza kuwa, mikakati hiyo imekuwa ikitekelezwa kwa njia ya huduma mbalimbali zikiwemo miradi inayotekelezwa na serikali kupitia wizara na halmashauri za wilaya.

“Miradi hii imekuwa chachu katika kufungua fursa na kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya kilimo, pia inalenga kuongeza uzalishaji na tija kama uboreshaji miundombinu ya umwagiliaji, miradi ya kuongeza thamani ya mazao kama vile viwanda vidogo, maghala, majosho, masoko na mingine mingi,”amefafanua Dkt.Mwita.

Wakati huo huo, Dkt.Mwita akiangazia upande wa Sekta ya Mifugo amesema, inachangia asilimia 7.4 ya pato la taifa, ikitoa ajira kwa takribani asilimia 36 ya watanzania na kuchangia wastani wa asilimia 22 ya mapato
ya kaya.

“Idadi ya mifugo iliyopo nchini, inaipa, Tanzania nafasi ya tatu barani Africa kwa wingi wa mifugo. Utekelezaji wa mikakati, ikiwemo ASDP II na Mpango kabambe wa Sekta ya Mifugo (Tanzania Livestock Master Plan), unaainisha
vipaumbele vitakavyoleta mabadiliko katika sekta ili kuchochea ongezeko la ajira, lishe na pato la taifa. Vivyo hivyo, Sekta ya Uvuvi inachangia asilimia 1.4 ya pato la taifa,ikitoa ajira kwa takribani asilimia 35 ya wantanzania wanoishi vijijini,”amesema.

Mbali na hayo, Dkt.Mwita amesema, licha ya kuwepo mikakati hiyo bado sekta ya kilimo inakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo uwekezaji mdogo, hii ikiwa ni kwa mujibu wa uchambuzi wa bajeti uliofanywa na ANSAF (2019/2020).

Amesema, kwa mujibu wa uchambuzi wa bajeti pia ulibaini kuwa kuna mahusiano chanya kati ya uwekezaji kwenye
sekta ya kilimo na ukuwaji wa sekta hiyo.

“Hivyo zinahitajika juhudi za haraka, kwani uwekezaji kwenye sekta ya kilimo ngazi ya halmashauri kupitia vyanzo
vya ndani inaonyesha wazi kuwa, halmashauri zinategemea kilimo kwa ajili ya mapato, lakini kiasi kinachotolewa na halmashauri kuendeleza sekta ya kilimo ni kidogo sana na halmasahuri nyingine hazitengi kabisa,”ameongeza Dkt.Mwita.

Katika warsha hiyo ya siku mbili, wadau hao wakiwemo madiwani, maafisa kilimo, watendaji kutoka mikoa mbalimbali nchini waliazimia kushirikiana kwa karibu na vyombo vya habari ili kuwezesha fursa za kilimo, ufugaji na uvuvi zilizopo katika maeneo yao zinatambulika na penye changamoto au mafanikio yaweze kuripotiwa ili koungeza hamasa ya uzalishaji wenye tija kwa manufaa ya jamii na Taifa kupitia sekta hizo.