December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Mwinyi:Tantrade fanyeni utafiti wa bidhaa zinazoletwa kwenye maonesho ya Sabasaba

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar es Salaam

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, ameitaka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania TANTRADE, kuhakikisha inafanya tafiti zenye tija kwa bidhaa zinazotumika kwenye maonesho ili kuongeza mapato na kukuza uchumi wa nchi hususani katika maonesho yajayo ya 48.

Rais Dkt. Mwinyi, ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam, wakati akifunga maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa, maarufu kama Sabasaba, ambayo yalianza rasmi Julai 28 na kufikia kilele Julai 13 mwaka huu.

Amesema, taasisi hiyo ikijiwekea misingi utaweza kufanikiwa zaidi katika maonesho yajayo mwakani na yatakuwa yameongeza washiriki wengi kutoka ndani na nje ya nchi.

Aidha Dkt. Mwinyi amesema,maonesho ya mwaka huu, yamefanikiwa zaidi kuliko maonesho mengine ya Sabasaba yaliyopita, kutokana na ushirikiano wa Serikali zote mbili ya Tanzania Bara na Serikali ya Zanzibar pamoja kwa kufungua masoko katika maeneo mbalimbali na utoaji wa elimu zaidi kwa washiriki wa maonesho hayo.

Pia ameipongeza TANTRADE pamoja na wadhamini wakuu wa maonesho hayo kwa mwaka huu ambao ni East Africa Commercial and Logistics -LACLC ya nchini China.

Pia ametoa wito kwa wazalishaji na wafanyabiashara kufanya biashara zenye tija hasa za kuhudumia mahitaji ya bidhaa wanazopokea na kuzalisha bidhaa zenye kiwango na ubora wenye uhakika.

Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda kutoka Zanzibar, Omary Said Shaban, amesema maonesho hayo ya biashara ni moja ya nyenzo muhimu inayosaidia kukuza sekta ya biashara nchini.

Amesema maonesho hayo yanatoa fursa kwa washiriki kutoka ndani na nje ya nchi, kutambulisha bidhaa au huduma mpya zilizopo sokoni.

Pia ametumia nafasi hiyo kumuhakikishia Rais kuwa, maonesho kama hayo ili wafanyabiashara na wajasiriamali kutoka Zanziba nao waweze kunufaika.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, Latifa Khamis, amelipongeza Jeshi la Polisi nchini, kuimarisha hali ya ulinzi na usalama kwenye maonesho hayo na pia kuwachukulia hatua waliyofanya vitendo vya wizi kwa waliyokuwa wanatembelea maonesho hayo.