Na Is-Haka Omar, TimesMajira,Online Zanzibar
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dkt.Hussein Ali Mwinyi, amesema endapo atakuwa rais wa Zanzibar atahakikisha anajenga bandari mpya ya kisasa ya mafuta na gesi asilia ili kukuza uchumi wa nchi.
Amesema ujenzi wa bandari hiyo hautoathiri shughuli za wananchi hasa wanaojishughulisha na uvuvi katika maeneo ya wilaya hiyo.
Ahadi hiyo ameitoa katika mwendelezo wa mikutano ya kampeni za CCM katika wilaya ya Kaskazini ‘B’ uliofanyika leo katika Shule ya Bumbwini Unguja.
Amesema bandari hiyo ikikamilika itakuwa ndio kitovu cha uchumi wa nchi, kwani itasaidia kutoa ajira nyingi.
Aidha, amesema atavipa kipaumbele vikundi vya ujasiriamali kwa kuvipatia mikopo na mafunzo ili wanufaike na fursa hizo. Aidha, alisema atahakikisha wananchi wa wilaya hiyo wananufaika na ufugaji wa kisasa wa samaki ili waende sambamba na dhana ya uchumi.
Pia amejiombea kura na kuwaombea kura wagombea wote wa CCM ili CCM iendelee kuongoza dola. Pamoja na hayo, aliwataka wananchi walinde amani ya nchi na wasikubali kuchokozeka na vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wapinzani.
Amesema hospitali ya wilaya, kununua vifaa tiba vya kisasa na kuajiri wafanyakazi wa sekta ya afya ili huduma zitakazotolewa zikidhi mahitaji ya wakaazi wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja.
Pia ameahidi kujenga barabara ya Bumbwini hadi Mahonda ili kukuza uchumi wa wananchi wa maeneo hayo. Aidha alisema watajenga shule ya ghorofa na daharia pamoja na kudhibiti changamoto ya wizi wa mifugo ili wananchi wanufaike na fursa za ufugaji.
Naye Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein, alisema historia ya Zanzibar imeanzia mbali kwani tangu utawala wa Wareno na waoman waliotawala Zanzibar kwa mabavu nao kisha waliondoshwa.
Dkt.Shein, amesema tangu mwa 1957 zilifanyika chaguzi mbalimbali, lakini wazawa hawakuwahi kushinda uchaguzi huo kutokana na kuwepo kwa njama za ukandamizaji.
Amesema baada ya utawala wa ukandamizaji wa wakati huo,Wazee wa kiafrika chini ya uongozi wa marehemu Abeid Amani Karume wakaamua kuondosha utawala huo kupitia mapinduzi ya mwaka 1964.
Dkt.Shein, alisema baada ya mapinduzi hayo nchi ilikuwa huru na kuweka viongozi kwa awamu mbalimbali toka awamu ya kwanza mpaka hivi sasa wanaelekea awamu ya nane.
Amesema kuna baadhi ya viongozi wa kisiasa wanajifanya hawatambui mapinduzi kutokana na sababu zao za kisiasa. Aliongeza kuwa kwa sasa nchi ipo katika harakati za uchaguzi, hivyo wananchi, wasikubali kuongozwa na watu wabaguzi wa kidini, kikabila na kisiasa.
“CCM imemteua Dkt.Mwinyi kwa kuwa ana sifa zinazokubalika ndani ya jamii sambamba na kuwa na sifa za ziada za kuwa mpole,mvumilivu,mcheshi, mcha Mungu na mwadilifu,”alisema.
Amesema Dkt.Hussein, ana sifa nyingine tofauti na wagombea wengine kwani ana uzoefu wa kiutendaji ndani ya Serikali na ni msomi wa fani ya udaktari.
Ameeleza kuwa CCM imemkabidhi Dkt.Mwinyi, bendera na ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/2025 ili vimuongoze katika kusimamia maslahi ya CCM.
Dkt.Shein, amesema ushindi wa CCM wa mwaka huu ni mkubwa ambao utakuwa ni wa kihistoria katika siasa za Afrika Mashariki, kwani CCM imejipanga vizuri kuhakikisha inashinda kwa njia za kidemokradsia.
Amesema hakuna njia ya mkato ya kuingia Ikulu na kwamba ni lazima chama kishinde kupitia uchaguzi huru na wa haki.
Aliwaombea kura za ndio wagombea wote wa CCM wakiwemo wagombea wa nafasi za Urais,wabunge,wawakilishi na madiwani
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
27 kulipwa kifuta jasho Nkasi
Mwakilishi Mkazi wa UN nchini awasilisha hati