Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Arusha
Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi amesema wanajivunia kuwa na taasisi za fedha imara zikiongozwa na benki ya CRDB, kwani kwa upande wa Zanzibar, benki hiyo imekuwa mshirika muhimu katika kuimarisha dhana ya uchumi wa buluu.
Kwani kupitia programu za uwezeshaji kama vile ‘INUKA na Uchumi wa Buluu’, benki hiyo imechangia sana katika kuendeleza sekta mbalimbali kama vile utalii, kilimo, ufugaji, uvuvi, mafuta, biashara na ujasiriamali.
Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Mei 17, 2024 wakati anafungua semina ya Wanahisa wa benki ya CRDB iliyofanyika ukumbi wa Simba, Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC) jijini Arusha.
“Kama mnavyoelewa fedha ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya Taifa letu,hivyo basi sekta ya fedha imara ni nguzo muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu, kwa sababu hii, Serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa katika kuhakikisha kuwa sekta hii ina mchango mkubwa katika maendeleo yetu,”ameeleza Dkt.Mwinyi.
Aidha Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa benki hiyo inashirikiana vyema na Serikali katika kuchochea ukuaji wa sekta ya michezo, ikilenga kutengeneza ajira kwa vijana kupitia vipaji vyao,wanathamini sana mchango wao huo katika kukuza uchumi wa Zanzibar na kuwaletea maendeleo Wazanzibari.
“Kumekuwa na ushirikiano mzuri na taasisi zetu za Serikali ambapo tumeshuhudia uunganishaji wa mifumo ya ukusanyaji wa kodi na tozo za Serikali, jambo ambalo limeongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato,tunathamini sana mchango wenu huu katika kukuza uchumi wa Zanzibar na kuwaletea maendeleo Wazanzibari,”
Sanjaru na hayo amesema ni matumaini yake benki hiyo itaridhia ombi la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Fedha na Mipango wa Zanzibar Dkt. Saada Mkuya kuwa Mkutano Mkuu wa 30 wa Wanahisa ufanyike Zanzibar mwakani.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Abdulmajid Nsekela amesema dhamira na utayari aliouonesha Rais Dkt. Mwinyi tangu anaingia madarakani mwaka 2020,benki hiyo imekuwa mdau muhimu katika maendeleo ya Zanzibar na Wazanzibari kwa kujenga ushirikiano wa kimkakati ambao umekuwa na manufaa.
“Upo usemi wa Kiswahili unaosema ‘Unayeokota naye kuni ndio utakayeota naye moto’, ni katika muktadha huu ambao umejengwa katika misingi ya ushirikiano, ninajivunia kusema kuwa CRDB imekuwa benki kiongozi katika kuwezesha uchumi wa Zanzibar kwa kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo hususani katika kuwawezesha wananchi kunufaika na fursa za uchumi wa buluu,”ameeleza na kuongeza
“Pamoja na uwezeshaji huo ambao tumekuwa tukiufanya kama benki, lakini kwa pamoja tumeweza kutekeleza programu ya pamoja ya ‘INUKA na Uchumi wa Buluu’, ambayo imeweza kuwafikia wajasiriamali wengi Zanzibar kwa kuwapatia mitaji na nyenzo muhimu za kukuza biashara zao,”.
Nsekela amesema kumekuwa pia na ushirikiano mzuri katika kusaidia kuimarisha ufanisi katika ukusanyaji wa mapato kupitia mifumo yao ya kidijitali ambayo wameweza kuunganisha katika taasisi mbalimbali za umma ikiwemo Mamlaka ya Bandari na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) ambao ni wanahisa wao.
“Kwa upande wa Zanzibar, benki yetu ina matawi manne, mawili Unguja na mawili Pemba,tuna CRDB Wakala zaidi ya 350, ATM zaidi ya 20 ikiwemo ATM ya kubadili fedha za kigeni (Forex ATM), vifaa vya manunuzi (PoS) zaidi ya 500 na biashara zinazopokea malipo ya msimbomilia yaani QR Code zaidi ya 200,”.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo Dkt. Ally Laay amesema Juni 2009,CRDB iliorodheshwa kwenye Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) ili kuuza hisa zake, ambapo hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2023, umiliki wa Serikali na Watanzania mmoja mmoja katika benki hiyo ni takribani asilimia 80.
Hivyo kufanya benki hiyo kuwa ya kizalendo, kwani mbali na kuongozwa na Watanzania wenyewe lakini hata umiliki wake kwa sehemu kubwa upo chini ya Watanzania.
Ambapo ameeleza kuwa umiliki huo pia umegusa pande zote mbili za Muungano, kwani umiliki wa Serikali kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii inahusisha Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) ambao wanamiliki hisa zaidi ya milioni 41 ambazo ni takribani asilimia 1.6 za hisa zote za benki ya CRDB.
“Umiliki wa ZSSF umekua ukiongezeka katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, ambapo mwaka 2021 ulikua asilimia 0.03, mwaka 2022 ulikua asilimia 1.4 na mwaka jana (2023) ukafika asilimia 1.6,” amesema Dkt. Laay.
More Stories
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili