January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Mwinyi aipongeza Ofisi ya Rais-Utumishi

Na James Mwanamyoto

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuifuatilia kwa karibu mipango ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) ili kuhakikisha inawanufaisha wananchi walio wengi hapa nchini.

Ameyasema hayo leo Ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Omary Mchengerwa akiwa na ujumbe wake wa viongozi wanaosimamia masuala ya TASAF, MKURABITA na Ajira katika Utumishi wa Umma waliofika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha.

Katika maelezo yake, Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, kwa vile Zanzibar ni ndogo ikilinganishwa na Tanzania Bara anaimani kwamba mafanikio zaidi ya Mipango ya TASAF na MKURABITA yatafikiwa kwa haraka zaidi.

Amesisitiza haja ya changamoto zilizokuwepo kufanyiwa kazi sambamba na mafanikio yaliopo kuelezwa ili yajulikane.

Kwa upande wa ajira Rais Dkt.Mwinyi ametoa shukurani kwa Waziri huyo kwa jinsi anavyolifuatailia suala hilo na kumpongeza huku akimtaka kuendelea kuhakikisha mafanikio zaidi yanapatikana kutokana na taratibu zilizoanza kuwepo.

Rais Dkt.Mwinyi ameeleza haja kwa Zanzibar kujifunza kutoka Tanzania Bara jinsi wanavyofuatilia shughuli hizo pamoja na taratibu za kufanya usaili pamoja na kuwa na danzi data za kutosha hali ambayo inapunguza usumbufu kwa wanaoomba ajira.

Amesema kuwa, utaratibu mpya uliopangwa ana matumaini makubwa kwamba utaleta mafanikio makubwa na kusisitiza haja ya kubadilishana uzoefu hatua ambayo itapelekea pande zote mbili za Muungano kufanikiwa.

Rais Dkt.Mwinyi alipongeza hatua zilizofikiwa ikiwa ni pamoja na jinsi ya mgawanyo wa mkopo wa fedha unavyofanyika katika mipango ya TASAF sambamba na hatua zinazochukuliwa katika MKURABITA na kueleza jinsi mashirikiano mazuri yaliyopo.

Awali Waziri Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Omary Mchengerwa amemueleza Rais Dkt.Mwinyi kwamba wizara yake imekusudia kutekeleza malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na yale yaliyokusudiwa katika Katiba yanafanyiwa kazi kwa vitendo.

Ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika miradi ya TASAF kwa upande wa Zanzibar huku akieleza namna ya mgao wa ajira unavyofanyika na kueleza changamoto zilizopo katika suala la ajira na namna zinavyofanyiwa kazi hivi sasa .

Amesema kuwa, kuanzia sasa wizara hiyo itakwenda sambamba katika michakato yote ya ajira ili kwa upande wa Zanzibar zifahamike pamoja na ushiriki mzuri uwepo.

Amesema kuwa, kwa upande wa Zanzibar katika masuala ya TASAF yameenda vizuri na kueleza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuhakikisha kwamba kaya zote hapa nchini zimefikiwa kwa azma ya kila Mtanzania aweze kufikiwa.

Aidha, Waziri Mchengewra ameipokea rai ya Rais Dkt.Mwinyi ya kutaka kupatikane kwa mafunzo sambamba na kubadilishana uzoefu kwa watendaji katika masuala ya ajira na utulimishi wa Umma kutoka Zanzibar kwenda kujifuza Tanzania Bara.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Ladislaus Mwamanga amesema kuwa, mfuko huo ulianzishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2000 kama mojawapo ya mikakati ya Serikali katika kupambana na umasikini kwa kutumia dhana ya ushirikishaji jamii na kutatua kero zao.

Amesema kuwa, awamu ya kwanza ya TASAF, umetekelezwa katika maeneo 42 zikiwemo halmashauri 40 za Tanzania Bara na Zanzibar na kutekelezwa kwa mafanikio makubwa katika huduma za elimu, maji, afya na nyenginezo ambapo jumla ya iradi 1,704 yenye thamansi ya TZS Bilioni 72 ilitekelezwa.

Ameongeza kuwa, utekelezaji wa TASAF Awamu ya Pili ulifanyika kwa kipindi cha miaka minane kuanzia mwaka 2005 hadi 2013 na jumla ya miradi 12,347 katika sekta mbali mbali yenye thamani ya TZS Bilioni 430 ilitekelezwa kwa ajili ya kutatua kero za wananchi.

Alisema kuwa, katika Awamu ya Tatu ya TASAF ambayo ilipangwa kutekelezwa kwa miaka 10 yenye vipindi viwili viwili ambapo jumla ya TZS Bilioni 430 zilitumika.

Mkurugenzi huyo alieleza kuwa kipindi cha kwanza kilihusisha Vijiji, Mitaa na Shehia 9,960 ambazo ni silimia 70 zilifikiwa na asilimia 30 zilizobaki zitafikiwa katika kipindi cha Pili ambacho kinatarajiwa kumalizika Julai 2021 na kutumia trilioni 2.03.

Kwa upande wa Zanzibar alisema kuwa miradi 75 yenye thamani ya Bilioni 3.0 ilitekelezwa katika awamu ya kwanza na awamu ya Pili miradi 814 yenye thamani ya Bilioni 8.8 ilitekelezwa katika kipindi cha kwanza cha Awamu ya Tatu ya utekelezaji wa Mpango ambapo Shehia 204 zilitekeleza miradi ya Bilioni 45 na kwa kipindi cha Pili utekelezaji ndio umeanza na Bilioni 112.87 zimetengwa kwa Wilaya zote na Shehia za Zanzibar kwa miaka minne ijayo mpaka 2023.

Nae Xavier Daud, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma alieleza majukumu ya sekretarieti hiyo huku akieleza jinsi ya vikao vya pamoja vinavyokaliwa ambapo kikao cha Aprili 21, 2011 kilieleza namna ya kutatua changamoto za Muungano hususan eneo la ajira katika utumishi wa umma.

Alieleza kwamba katika vikao hivyo ilikubalika kuwe na uwiano wa ajira kwa taasisi za Muungano ambapo ilikubalika kuwa Tanzania Bara iwe na asilimia 79 na Tanzania Zanzibar iwe na asilimia 21 ya nafasi za ajira kila zitakapotangwazwa.

Katibu huyo alitoa shukurani kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwapatia ofisi yenye dhamana na Utumishi wa Umma Zanzibar ajira zipatazo 92 zilitolewa kwa Wazanzibari ambapo kwa taasisi za Muungano ni 42 na taasisi binafsi ni 50 kuanzia Julai 2015 hadi Machi 2021.

Dkt.Seraphia Mgembe Mkurugenzi Mkuu MKURABITA alieleza shughuli ilizozitekeleza ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo kwa ajili ya urasimishaji wa ardhi vijijini ambapo kwa upande wa Zanzibar viwanja 4,600 vimepimwa na hati za matumizi ya ardhi 116 zimetolewa na zinaendelea kuandaliwa.

Alieleza shughuli nyingine ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa urasimishaji wa biashara, kuwajengea uwezo wananchi wa namna ya kutumia hati miliki za rasilimali walizorasimisha.