Na Mwandishi Wetu, timesmajira, online Pemba
CHAMA cha Mapinduzi jana kimezindua kampeni zake Kisiwani Pemba baada ya Septemba 12 kuzindua kampeni kisiwani Unguja na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa watu.
Akiwahutubia maelfu ya wananchi na wanachama wa CCM katika viwanja vya Gombani Chake Chake Pemba, Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein alisema kuwa mgombea wao wa urais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi ni chaguo la CCM na chama hakikubahatisha kumchagua yeye.
Alisema CCM Zanzibar itashinda kwa kishindo katika uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu na wananchi hawatofanya makosa watakichagua chama hicho.
“Wembe ni ule ule wakitaka watanyolewa wasipotaka watanyolewa “alisema Dkt. Shein.
Alisema kuwa mgombea wa Dkt. Hussein ana uwezo mkubwa wa kuiongoza Zanzibar hivyo aliwataka wananchi kumpigia kura katika uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Alieleza kuwa kiongozi huyo ana uwezo mkubwa na ni mtu mwenye maadili na mchapa kazi mahiri na anaejituma .
“Sisemi haya kwa kumtengenezea sifa nasema haya ndiyo aliyonayo mgombea wetu ni mtu mwenye maadili,nidhamu na heshima yake haina shaka”alisema Dkt. Shein.
Alieleza kuwa sifa alizonazo mgombea huyo,wagombea wengine wa vyama vya siasa hawana,ambapo Dk Hussein si mtu jeuri hana kiburi wala hana tabia ya kuropokwa ovyo.
Akizungumza kwa niaba ya wagombea Ubunge,Uwakilishi na udiwani kisiwani Pemba Profesa Mbarawa Mnyaa,alisema wazanzibari hasa pemba wanataka maendeleo na uchaguzi wa mwaka huu Pemba itakua historia kwa CCM.
“Dalili ya Mvua ni mawingu Pemba mwaka huu tutaandika historia “alisema Mnyaa ambae mgombea ubunge jimbo la Mkoani Pemba.
Naye Mgombea Urais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi,alisema endapo atapata ridhaa za wananchi atahakikisha maisha ya wananchi yanakua mazuri.
Alieleza kuwa ataendeleza yote mazuri yaliofanya na serikali ya awamu ya saba ikiwemo elimu,afya bure na huduma zengine muhimu kwa ajili ya maendeleo ya Zanzibar.
Alisema amedhamiria kufanya kazi kubwa ya maendeleo ya kiuchumu wa kisasa. Alisema ili kuyafanya maisha ya wananchi kuwa bora ni kukuza uchumi ikiwemo uvuvi,utalii na viwanda.
Alisema kuwa Pemba kuna fursa nyingi na vivutio vingi lakini idadi ya watalii wanaofika ni ndogo hivyo atakuza sekta hiyo ili uchumi kukua.
Aidha alisema akiyafanyia kazi maeneo ya kiuchumu maisha yatakua mazuri lakini miundombinu ya kisasa itarahisisha kazi hiyo ya ukuaji wa uchumi.
“Uchumi lazima uendani na uboreshaji wa huduma za jamii ikiwemo elimu,afya na huduma za maji safi na salama “alisema Mgombea huyo.
Alieleza uchumi huo utatoa fursa nyingi za ajira hivyo aliwataka vijana kua tayari kuendana na uchumi mpya.
Akizungumzia kuhusu kilimo alisema idadi za tani za karafuu na mwani ni ndogo hivyo lazima kuweka nguvu katika maeneo hayo ili uzalishaji uwe mkubwa.
Dkt Mwinyi alisema maendeleo hayataweza kupatikana bila ya amani na utulivu hivyo kuendelea kudumisha amani.
“Tusitoe nafasi suala la ubaguzi lazima kupiga vita na kuwa wamoja,”alisema.
Alisema huwezi kuwa na uchumi wa kisasa kama hakutakua na utawala bora na kupinga vita rushwa,ubadhilifu wa mali,udhalilishaji na dawa za kulevya.
Alisema atasimamia Maslahi ya nchi katika mashirika mbalili mbali ikiwemo jumuiya ya afrika mashariki. Mgombea huyo aliwataka wananchi kumpa kura nyingi za ndio ili kuweza kushinda katika uchaguzi mkuu.
“Tusibweteke tujitokeze kwa wingi kupiga kura na mara hii kusiwe na manung’uniko yoyote katika ushindi wa CCM “alisema. Uzinduzi huo ulitumbuizwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii kutoka Zanzibar na Tanzania bara.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
27 kulipwa kifuta jasho Nkasi
Mwakilishi Mkazi wa UN nchini awasilisha hati