December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwakyembe ahimiza maadili kumuenzi Nyerere

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

WAZIRI wa zamani na mwanasiasa Harrison Mwakyembe, amewataka vijana kulinda na kuthamini Muungano, huku akiwasisitiza kuishi na kusimamia maadili ya Kitanzania ikiwa ni kuenzi maono ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, kwasababu bila kufanya hivyo kutasababisha kuwe na taifa mfu.

Amesema Muungano ndio tumaini pekee lililosababisha kuwepo kwa umoja, usalama, ulinzi, kuchochea maendeleo katika sekta binafsi, biashara na kukua kwa uchumi.

Mwakyembe aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana katika Mdahalo wa Kitaaluma wa Chuo Cha Ustawi wa Jamii (ISW), uliyobebwa na mada isemayo ‘Maadili ya Vijana kwa Jamii’ ikiwa ni maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano.

“Tujivunie Muungano wetu na sio kwa bahati nasibu tuwe kifua mbele, tujivunie na kuulinda Muungano ndio maana mwalimu alisema hata bila mapinduzi Tanganyika na Zanzibar ingeungana,nchi kubwa zilikiwa haziamini kama Muungano huu utadumu.

“Tulinde maadili yetu sisi ndio tunatakiwa kupaza sauti, nashukuru serikali kwa kuendelea kuchukua hatua kufungia vitabu 16 vilivyo kinyume na maadili ,”alisema.

Aidha Mwakyembe aliwataka vijana wahakikishe wanapata historia sahihi ya taifa kuhusu maadili kwa lengo la kutopotoshwa na kuiga maadili kutoka nje ya nchi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho Sophia Simba, alisema wanafunzi wa chuo hicho na maofisa ustawi wa jamii nchini wanakazi kubwa ya kutengeneza mikakati na njia sahihi ya kukabiliana na mmomonyoko wa maadili.

“Hii ni fursa kwenu watu wa ustawi wa jamii mtengeneze mikakati ya kuishawishi serikali kwa namna gani tunakabiliana na suala la mmonyoko wa maadili na kulirejesha taifa letu katika misingi bora ya maadili,”alisema

Pia Sophia alisema, jamii ifuate misingi bora ya malezi, na wafanye ufuatiliaji wa kutosha wa makuzi ya watoto, kwasababu itasaidia kujenga ustawi mzuri wa taifa.

Naye Mkuu wa chuo cha ISW Dk. Joyce Nyoni alisema taifa likiwa na maadili mema litazidi kudumisha hata Muungano uliyopo.

Alisema mdaharo uliyofanyika chuoni hapo umelenga kuikumbusha jamii kuhusu masuala ya maadili, kwani ni jambo la muhimu katika kuhakikisha taifa linakuwa na ustawi bora.

“Tunasheherekea Muungano lakini tunaendelea kusisistiza maadili ni muhimu ili tuweze kustawisha jamii na Muungano wetu ambao tumeendelea kujivunia kwa kiasi kikubwa,”alisema.

Alisema ni muhimu vijana kushiriki katika kuenzi maadili ya Kitanzania kwasababu hao ndio nguvu kazi ya taifa.

Kwamujibu wa Dk. Nyoni jamii, viongozi wa dini taasisi za elimu wanawajibu wa kusimamia ipasavyo suala la maadili ili kujenga kizazi bora.

Naye mmoja wa watoa mada katika kongamano hilo Mtaalamu wa Saikolojia Dk. Zainabu Rashid, alisema ili kulinda maadili ni wajibu wa wazazi kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji wa kutosha watoto wao kuanzia nyumbani hadi shuleni.