Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango ameongoza sherehe za miaka 58 za muungano wa Tanzania zilizoambatana na uzinduzi wa kitabu ambacho kinazungumza misingi ya muungano na maendeleo yake na kwamba kitabu hicho ni kitabu pekee tangu muungano ulipoanzishwa.
Akiongea kwenye maadhimisho hayo jijini hapa leo ,Dkt.Mpango amesema Muungano kati ya Tanzania bara na Zanzibar umezaa mafanikio makubwa ikiwemo muingiliano wa pande hizo mbili na kwamba hali hiyo inajidhihirisha wazi kuwa hiyo ni zaidi ya hati ya muungano na orodha inayohusu mambo yote ya muungano.
Amesema,wananchi wa pandezote mbili wamepiga hatua na kasi ya ushirikiano wa kibiashara na kuinua uchumi na kwamba hatakuwa mpole kwa wale wote watakaojaribu kuuchezea Muungano.
Mbali na faida hizo,amesema zipo faida nyingi zinazoonekana wazi na zile zisizoonekana katika Muungano na hivyo kuufanya kuzidi kuimarika.
Kwa takwimu zilizopo, Watanzania walio wengi wamezaliwa baada ya Muungano, Kwa mantiki hiyo, wananchi wengi na hasa vijana wanaufahamu Muungano huu ama kwa kusimuliwa au kusoma machapisho mbalimbali.
Aidha, kumekuwepo mijadala mingi kuhusu historia, mantiki ya aina ya muungano wa nchi zetu mbili, faida na changamoto zake.
“Kupitia mijadala hii inaonekana kuwa wananchi wengi hawana uelewa mpana kuhusu Muungano wetu,hivyo, kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu kuhusu Muungano wetu na Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuendelea kuelimisha zaidi wananchi juu ya muungano.
Dkt. Mpango ameongeza kuwa Muungano huu ni wa watu hivyo ni Muungano unaoishi ili kutimiza matakwa na malengo ya wananchi wake na licha ya mafanikio mengi yaliyopatikana zilikuwepo pia changamoto mbalimbali ambazo zilijitokeza kwa nyakati tofauti na kufanyiwa kazi.
Pia amesisitiza kuwa changamoto hizo hazimaanishi kuwa Muungano wetu sio imara au hauna manufaa kwa wananch bali jambo la kufurahisha ni kwamba Serikali za pande mbili zimekuwa zikibainisha changamoto hizo na kufanya jitihada ili kuzipatia ufumbuzi.
Hata hivyo amezitaja faida ambazo zimepatikana kipindi cha miaka 57 ya Muungano kwa pande zote mbili kuwa ni pamoja na kuimarika kwa udugu wa damu miongoni mwa wananchi, kudumu kwa umoja na mshikamano wa kitaifa.
Faida nyingine ni kuimarika kwa ulinzi na usalama, kukua na kuimarika kwa biashara na shughuli nyingine za kiuchumi na fursa ya kutumia rasilimali zilizopo kwa pamoja ikiwemo ardhi na bahari.
Pia amesisitiza Serikali za pande mbili chini ya uongozi wa Awamu ya Sita Bara na Awamu ya Nane Zanzibar zimeweka suala la kuimarisha Muungano kuwa ni moja ya vipaumbele vyake na hivyo zinaendelea kushirikiana kwa pamoja kuhuisha na kudumisha muungano.
Pamoja na kumuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Selemani Jafo kumpatia taarifa ya kongamano hilo na mapendekezo yake ili ayafanyie kazi katika kuimarisha utekelezaji wa masuala ya Muungano.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo amesema wamefanikiwa kutatua kero 18 za muungano kati ya 25 zilizopo.
Amefafanua kuwa mwaka 2020 waliweza kutatua kero saba na kubaki kero 18 za muungano.
“Lakini kwa uongozi wenu wewe (Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango) na mheshimiwa Rais (Rais Samia Suluhu Hassan) tumefanikiwa kutatua kero 11 (mwaka 2021) na hivyo ukijumlisha na zile saba zinakuwa 18,”amesema.
Amesema katika sherehe hizo Dk Mpango anazindua kitabu ambacho kinazungumza misingi ya muungano na maendeleo yake na kwamba kitabu hicho ni kitabu pekee tangu muungano ulipoanzishwa.
“Maelekezo yenu yamefanikisha hili, kitabu hichi kitakuwa ni nyenzo kwa Watanzania, nyenzo kwa wadau mbalimbali ya msingi, historia na maendeleo ya muungano katika miaka mbalimbali,”amesema.
Amesema kama itampendeza kinaweza kutumika katika somo la historia shuleni ili kupandikiza agenda ya ufahamu kuhusu muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam